Na WINFRIDA MTOI, DAR ES SALAAM
KLABU ya Simba imeweka bayana kuwa hakuna timu yoyote Tanzania inayoweza kumsajili kiungo wao Mzambia, Clatous Chama na ataendelea kubaki Msimbazi hadi pale atakapojisikia kuondoka nchini.
Kauli hiyo imekuja baada ya hivi karibuni kuibuka mijadala juu ya kufikia ukingoni kwa mkataba wake Julai mwakani na kiwango anachokionesha kwa sasa.
Pia hivi karibuni baada ya mechi yao na Biashara United, Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Sven Vandenbroeck, alisema endapo nyota huyo ataendelea kuwa na kiwango hicho kuna hatari ya kumkosa.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, ametolea ufafanuzi suala hilo, wakati alipotembelea ofisi za New Habari (2006) Ltd, wachapishaji wa magazeti ya MTANZANIA, DIMBA, BINGWA na RAI, alisema kuwa Chama haendi popote.
Alisema ni kweli mkataba wa mchezaji huyo unamalizika mwakani, lakini wanatarajia kumuongezea mwingine ili andelee kuwa raha mashabiki wa Simba.
Manara alisema katika hali ya kawaida na kiwango cha mchezaji huyo, hakuna klabu inayoweza kumsajili hapa nchini kwa sababu tayari mwenyewe alishaonesha mapenzi na Simba na kuozoea mfumo wa timu hiyo.
“Chama tutaongeza mkataba wake, pia niweke wazi hakuna Tanzania tofauti na Simba inayoweza kumsajili Chama, Yanga haiwezi kumsajili na haitaweza kusajili mchezaji wa aina ya Chama.
“Unadhani Chama akienda Yanga zile pasi za kisigino anaweza kumpigia nani na kufunga, Chama akiondoka Simba labda anakwenda kucheza kwao au timu nyingine za nje si Tanzania,” alitamba Manara.
Amtabiria makubwa Bwalya
Katika hatua nyingine Manara, alisema kiungo wao mpya, Larry Bwalya atakuja kufanya kitu kikibwa Simba ambacho kila mmoja atashangaa.
Manara alisema bado kuna watu hawajamuelewa Bwalya, lakini ni kati ya wachezaji wenye vipaji na viwango vya juu na kitu atakachokuja kufanya kila mtu atakumbuka kauli yake.
“Bwalya atakuja kuwapa kitu kikubwa Simba kama nilivyowahi kusema kwa Chama wakati anasajiliwa, watu wakaniona mjinga, lakini kile anachokifanya sasa maneno yangu yametimia,” alisema.
Manara amekiri kuwa waliipindua meza kwa Yanga kumnasa nyota huyo, licha ya kwamba watani zao hao waliahidi kutoa dau kubwa kuliko wao.
Alisema kilichoibeba Simba katika kumnasa Bwalya kirahisi ni ukubwa klabu hiyo na mafanikio ya Mzambia mwenzake, Chama kwenye kikosi hicho.
“Ukubwa wa klabu ya Simba ndiyo uliotufanya kumpata Bwalya, ni kweli Yanga walimtaka na walitangaza dau kubwa kuliko sisi, lakini ukubwa wa timu na mchezaji alipoangalia inashikiriki michuano ya Kimataifa ilikuwa rahisi,” alisema.
Alieleza kuwa kingine kilichorahisisha Bwalya kutua Simba ni ukaribu waliojenga na klabu ya Power Dynamos anayotoka mchezaji huyo.
Kameta naye aliwatoa jasho
Alisema kati ya wachezaji waliyoitoa jasho Simba hadi kunasa saini yake ni David Kameta ‘Duchu’, waliyemsajili kutoka Lipuli.
“Watu wanaweza wasiamini, lakini ukweli kati ya wachezaji waliotusumbua kuwapata katika usajili msimu huu ni Kameta kwa sababu alikuwa anatakiwa na timu nyingi, Simba tukaamua kufanya mawindo yetu kimya kimya,” alisema.