24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wanasiasa wawe makini na ndimi zao

Hii ni wiki ya nne tangu kampeni za siku 60 za Uchaguzi Mkuu zianze ambapo tayari vyama vinavyoshiriki wagombea wake wako maeneo mbalimbali kwa ajili ya kumwaga sera ili wachaguliwe.

Tunasisitiza kwa mara nyingine tena kila kundi linaloshikiri katika uchaguzi huu kuzingatia haki ili kutovuruga amani iliyopo kwa sababu kuna maisha baadaya uchaguzi.

Tunarudia kusisitiza jambo hilo kwa sababu wapo baadhi ya wagombea na wapambe zao ambao wamesikika katika majukwaa wakizungumza lugha zenye kuashiria  uvunjifu wa amani.

Ushahidi wa hilo ni kipande cha sauti kinachozungushwa kwenye mitandao ya kijamii ambapo anasikika mwanasiasa mmoja visiwani Zanzibar akizungumza lugha ambayo sisi tunaona ina kila dalili ya kukusudia kufanya uhalifu na uvunjifu wa amani.

Wagombea tunafahamu wapo kwenye kampeni za kutafuta kura ili waweze kuwaongoza  wananchi ni vyema wakatumia nafasi hiyo pasipo kuwatisha au kuwalazimisha kwa namna yeyote ile ikiwamo kuwapa rushwa wananchi ili wawachague.

Lakini pia ni vyema wakawa makini kwenye kauli zao, hekima ikatangulie kwa kile ambacho watakitenda na kukisema na kila anayehubiri amani afahamu kwamba msingi wake ni kutenda haki.

Sisi kama chombo cha habari kilicho na jukumu pamoja na mengine la kuelimisha tunasisitiza amani hasa katika kipindi hiki nyeti.

Amani inaweza kupotea kwa uzembe au hila hivyo kila kundi linaloshiriki uchaguzi ni vyema ikatambua thamani hiyo na kuilinda kwa udi na uvumba.

Wananchi wao kama wapiga kura wamebeba wajibu  mkubwa wa kudumisha amani hivyo wanapaswa kuwa makini kwa kutathimini na kuchuja yale wanayosikia kutoka kwa wagombea.

Ni vyema watambue kwamba wamebeba Taifa migongoni mwao hivyo kila wanaloliamua ama kulitenda wafanye hivyo kwa kuzingatia haki na amani.

Wananchi wanapaswa kuwa makini na kutojiingiza kwenye ushabiki usio na mantiki.

Vyombo vinavyohusika kusimamia uchaguzi kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Msajili wa vyama vya siasa, vyama siasa na vyombo vya dola navyo vitekeleze wajibu wake kwa misingi ile ile ya kutenda haki.

Wale waliozoea kuminya haki kwa sababu ya mazoea ya kudhani Watanzania ni waoga hawapaswi kufanya hivyo tena kwasababu kuna kuchoka.

Vyombo vinavyosimamia uchaguzi vinapaswa kuongozwa na uaminifu, kutenda haki na kurebisha kasoro zinazojitokeza haraka ili uchaguzi uweze kufanyika kwa amani.

Vyombo hivi havipaswi kushiriki katika uonevu itakuwa ni kama vile kuwaweka Watanzania katika hali ya shaka na kufuta uaminifu.

Matokeo ya hayo yote yako wazi, hivyo kila mmoja asiwe mwepesi kuhubiri amani na wakati huo huo akijificha kwenye mwamvuli wa kutotenda haki kwa kuwa amani na haki ni kama chupa na mfuniko wake.

Asitokee yeyote ambaye atafanya hivyo akiamini Watanzania ni wajinga au waoga, kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake akiamini kuna maisha baada ya uchaguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles