GRACE SHITUNDU, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa zamani wa Mambo ya Nchi za Nje, Bernard Membe amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha ACT Wazalendo kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Membe ambaye alichukua fomu hiyo jana saa nane mchana pamoja na mambo mengine aliahidi kutema cheche siku chache zijazo wakati atakaporudisha baada ya kujaza kwa ukamilifu.
Hatua ya Membe kuchukua fomu imekuja ikiwa ni siku moja baada ya kutambulishwa rasmi kwa wanachama wa ACT-Wazalendo katika mkutano maalumu uliofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City jiji Dar salaam.
Membe aliyewasili katika ofisi ya chama hicho iliyopo Magomeni akiwa ameongozana na mke wake, Dorcas Membe.
Alipokelewa na wanachama wa chama hicho na kisha kukabidhiwa fomu hiyo na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu.
Mara baada ya kupokea fomu hiyo Membe alipata nafasi ya kuzungumzia na waandishi wa habari ambapo aliwashukuru wanachama wa chama hicho kwa mapokezi mazuri na kuahidi kuzungumza zaidi wakati wa kurudisha fomu hiyo.
“Nimefurahishwa na mapokezi niliyopata mimi na mke wangu, kubwa nililonileta ni kuchukua fomu kufuatia na ombi la Mwenyekiti, Maalim Seif Shariff Hamad na wanachama wa ACT la kuniomba nigombee kiti cha urais kupitia tiketi ya ACT Wazalendo.
“Leo asubuhi nimetekeleza kwa maandishi na nimekabidhi, ACT inakwenda chap chap, nimekabidhiwa fomu nitakwenda kuzisoma na nitazijaza kwa usahihi kwenye herufi kubwa nitaweka kubwa kwenye nukta nitaweka nukta ili asipite mdudu akasema sikujaza vizuri fomu hii”, alisema Membe.
Alisema pia anafurahi kuona ameanza kuchukua fomu hiyo na anaamini wengine watajitokeza kwani ACT ni chama cha demokrasia.
“Nimechukua fomu hii nitakwenda kuijaza na kama kuna la kusema nitasema siku ya kurudisha fomu, kwa leo ndugu zangu wanahabari tukubaliane kwamba nimeelemewa na huu mzigo kwa hiyo mniache niubebe niupeleke nyumbani kwangu nikajaze nitekeleze mambo yote halafu siku ya karibuni sana nitakaporejesha fomu hii nitamwaga cheche mbili tatu, vinginevyo asanteni sana”, alisema Membe.
Membe alihamia ACT Wazalengo Julai 7 mwaka huu na kutambuliswa rasmi jana ikiwa ni baada ya kufukuzwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi.