27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Bunge laikabidhi serikali shule ya wasichana

 RAMADHAN HASSAN– DODOMA

BUNGE limekabidhi shule ya kisasa ya wasichana iliyojengwa na wabunge huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiahidi kwa kusema kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika elimu kwa kuhakikisha ndoto za mtoto wa kike zinatimia ikiwemo kuwawezesha wale wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dodoma, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bunge ambayo imejengwa na wabunge kwa kushirikiana na Chama cha Wabunge Wanawake Tanzania (TWGP)

Waziri alisema kuwa elimu ndiyo msingi wa maisha, hivyo Serikali itaendelea kuhakikisha inawekeza kwa mtoto wa kike ili ndoto zake ziweze kutimia.

“Wito wangu katika shule hii ni lazima mtambue wanafunzi wasichanaa wenye vipaji ikiwemo wenye mazingira ya kawaida hatimaye kuongeza idadi ya watoto wa kike wenye utaalamu,” alisema.

Pamoja na hali hiyo, Majaliwa alisema kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa wale ambao watawapa mimba wanafunzi wa kike.

“Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa wale ambao watawapa mimba watoto wa kike, wakuu wa wilaya simamieni sheria. Kwa upande wa vyuo anzisheni madawati ya malalamiko na ninafurahi kwa sababu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amechukua hatua kwa wahadhiri ambao wamekuwa wakiwarubuni wanafunzi,” alisema.

Pia aliiitaka Tamisemi na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kusimamia vifaa vya majanga ya moto vinapatikana katika shule nchini.

“Ni vyema kukawa na ndoo za mchanga, Fire extinguisher pamoja na wanafunzi kupewa elimu kuhusiana na majanga ya moto katika shule za msingi na Sekondari,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema katika shule za sekondari kuwe na mwalimu wa kike ama wa kiume wa malezi na sio kuwa na wanaume pekee ama wanawake pekee.

 Vilevile alizitaka shule nchini kuhifadhi na kutunza mazingira kwa kupanda miti.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amemwagiza Mwenyekiti wa Kijiji cha Kikombo, Yona Kusaja kuorodhesha majina ya watu ambao wanadai kwamba hawajalipwa fidia kupisha ujenzi wa shule hiyo.

Hatua hiyo imekuja baada ya mwenyekiti huyo, kudai kwamba kuna baadhi ya wananchi wanamalalamika kwamba bado hawajalipwa fidia kupisha ujenzi wa shule hiyo.

Kwa upande wake,Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alisema shule hiyo itakuwa ni kwa ajili ya wanawafunzi wasichana wenye vipaji maalum kutoka katika maeneo mbalimbali nchini.

“Nalipongeza Bunge kwa kuacha alama tunashukuru kwa kutuunga mkono,tunaahidi kuienzi, na hata walimu wanaokuja hapa wamechaguliwa kwa umakini mkubwa,letu ni kuifanya shule hii kuwa miongoni mwa shule zenye vipaji Maalum kama vile Msalato, Kilakala, Tabora Girls,” alisema

Alisema waliunga mkono juhudi za Bunge kwa kutoa Sh milioni 200 kwa ajili ya kugharamia sehemu ya ujenzi huo.

Naye,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alisema wanafunzi 120 wameishachaguliwa kujiunga na shule hiyo ambapo mwalimu mkuu na walimu wengine nane wameishapatikana.

“Shule hii itakuwa ni ya mchepuo wa masomo ya Sayansi, tuna shule 158 za wawasichana nchini. Niwahakikishie sisi Serikali tutaendelea kuleta miundombinu hapa,” alisema.

Kwa upande wake Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema wanapendekeza shule hiyo iitwe Bunge ili kuonesha kwa vitendo jinsi ambavyo wabunge wameonesha jitihada ili shule hiyo ipatikane.

Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa Chama cha Wabunge Wanawake (TWGP), Margaret Sitta, alisema lengo la chama chao ni kujenga usawa wa kijinsia pamoja kutetea haki za watoto wa kike.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles