WASHINGTON, Marekani
JESHI la Anga la Marekani limefanikiwa kurusha roketi yake ya Atlas V katika anga za juu, huku ikiwa imeibeba ndege aina ya X-37B.
Ndege hiyo inaelezwa kwenda kufanya oparesheni za siri katika anga za juu.
Roketi hiyo ilirushwa Jumapili kutoka eneo la Cape Canaveral, ikiwa ni siku moja toka kuahirishwa kurushwa Jumamosi kutokana na hali mbaya ya hewa.
Ndege hiyo ambayo pia injulikana kama Orbital Test Vehicle (OTV), itatuma satelaiti katika mzingo wa dunia (orbit) na kujaribu tekmolojia mbalimbali katika eneo hilo la anga za mbali.
Hii ni safari ya sita ya kiuchunguzi kwa ndege hiyo katika anga za mbali.
Safari ya wakati huu imetunukiwa kwa wafanyakazi walio mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya virusi vya corona pamoja na walioathirika na virusi hivyo. Ujumbe maalumu uliojumuisha maneno “Marekani ni thabiti” yaliandikwa kwenye kichwa cha roketi.
X-37B ni mradi maalumu wa siri ambao ni vitu vichache tu kuuhusu vinavyojulikana. Makao makuu ya jeshi la Marekani, Pentagon, yametoa maelezo machache sana juu ya uwezo wa ndege hiyo iso rubani.
“Oparesheni hii ya X-37B itafanya majaribio mengi zaidi kuliko oparesheni nyengine yeyote ya awali,” Waziri wa Jeshi la Anga, Barbara Barrett alieleza mwanzoni mwa mwezi huu.
Moja ya majaribio yatakuwa ni athari ya mionzi kwa mbegu na vitu vingine.
Programu ya X-37B ilianza mwaka 1999. Ndege hiyo inafanana na ndege ndogo ambazo zilikuwa zikirushwa na binadamu katika anga za mbali ambazo zilistaafishwa rasmi mwaka 2011. Inaweza kurejea duniani kwa kushuka taratibu na kutua katika kiwanja cha ndege.
Ndege hiyo, imetengenezwa na Kampuni ya Boeing,inatumia umeme wa nguvu ya jua. Ina urefu wa futi 29 (sawa na mita 9), urefu wa mabawa yake ni takribani mita 15 na ina uzito wa kilo 4,989 (tani 4.9).
Kwa mara ya kwanza ndege hiyo iliruka angani Aprili, 2010 na kufanya oparesheni yake anga za juu kwa miezi minane.
Safari ya mwisho ya ndege hiyo (kabla ya hii mpya),ilifikia tamati Oktoba, mwaka jana, baada ya kukaa anga za juu kwa siku 780.
Kwa ujumla mpaka sasa ndege imeshatumia muda wa zaidi ya miaka saba kufanya opereshenii zake za siri katika anga za mbali.
Haijulikani kwa safari hii ndege hiyo, itachukua muda gani kumaliza operesheni yake.