27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mfumo wa afya unaweza kuporomoka-meya

SAO PAULO, Brazil

Meya wa jiji kubwa zaidi nchini Brazili, São Paulo, Bruno Covas amesema  mfumo wa afya unaweza kuporomoka huku kukiwa na ongezeko la mahitaji ya vitanda vya dharura ili kuwahudumia wagonjwa wa corona.

Covas alisema hospitali za umma za jiji hilo zinaweza kujaa katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Sao Paulo, ni moja kati ya miji iliyoathirika zaidi nchini Brazil kukiwa na watu 3,000 waliopoteza maisha mpaka sasa kutokana na corona.

Jumamosi, Brazil ilizidi nchi za Hispania na Italia na kuwa taifa la nne lenye idadi kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya corona.

Wizara ya Afya imeripoti maambukizi mapya 7,938 katika kipindi cha saa 24, jumla ya watu walioambukizwa ikifikia 241,000.

Marekani, Urusi na Uingereza ndizo zilizo na idadi kubwa zaidi ya watu waliopatwa na maambukizi.

Idadi ya waliopoteza maisha katika nchi hiyo ya Amerika ya Kusini  kipindi cha saa 24, ni watu 485, ikiwa na jumla ya vifo 16,118, takwimu zinazolifanya taifa hilo kushika nafasi ya tano kati ya nchi zenye idadi kubwa ya vifo.

Wataalamu wa afya,wameonya idadi kamili ya walioambukizwa nchini humo inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko takwimu zilizotolewa na Serikali kutokana na upungufu wa vipimo.

Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro amekosolewa vikali ndani na nje ya nchi kwa namna anavyoshughulikia janga la corona linaloendelea kushika kasi.

Alipuuza ushauri wa wataalamu wa afya duniani kuhusu kutochangamana siku ya Jumapili, alipopiga picha na watu wanaomuunga mkono na watoto katika mji wa Brasilia.

Covas alisema sasa yuko kwenye mazungumzo kuhusu hali hii na gavana wa jimbo kwa ajili ya kuweka marufuku ya kutotoka nje ili kujaribu kupunguza maambukizi kabla hospitali hazijazidiwa.

Gavana wa Jimbo la Sao Paulo ana mamlaka kwa polisi na msaada wake utakuwa muhimu ikiwa amri ya kutotoka nje itakuwa ya mafanikio.

Sao Paulo ina jumla ya watu karibu milioni 12 na takwimu zinaonesha  wengi wa wakazi wa mji huo, wamekuwa wakikiuka sheria ya kutochangamana.

Jimbo la Sao Paulo lilianzisha utaratibu wa karantini karibu miezi miwili iliyopita -biashara, hospitali na maeneo ya umma yalifungwa na watu walitakiwa kukaa nyumbani.

Lakini hakuna adhabu yoyote kwa mtu atakayevunja sharia hizo. Wakazi wengi wa wamekuwa wakiendesha magari mpaka kwenye fukwe za bahari wakati wa mwisho wa juma.

Kutokana na hali hiyo paliwekwa sheria ya kuvaa barakoa ambayo nayo inapuuzwa mara kwa mara-watu walionekana wakiwa matembezini wakiwa hawana barakoa wengine wakiwa wamezivalia shingoni barakoa zao. Inaonekana kabisa kuwa ugonjwa huu hautiliwi maanani.

Wakati huohuo, watu wanashuhudia Ulaya ikifungua shughuli zake na kuna mashaka kitakachotokea nchini Brazil. Lakini kama Meya alivyozungumza mwishoni mwa juma, mji unapaswa kusimamisha shughuli zake kabla haujafunguliwa tena. Watu wengi wanatarajia kukabiliwa na masharti makali ya kutotoka nje katika majuma yajayo.

Rais Bolsonaro anashughulikia vipi janga hili?

Wiki iliyopita, Waziri wa Afya nchini Brazil, Nelson Teich alijiuzulu baada ya kuwa katika nafasi hiyo kwa kipindi cha chini ya mwezi mmoja.

Bwana Teich alijiuzulu baada ya kumkosoa waziwazi  Bolsonaro aliyeruhusu maeneo ya kufanyia mazoezi na maeneo ya saluni kufunguliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles