Ashura Kazinja, Morogoro
CHAMA cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Mkoa wa Morogoro, kimewaombawamiliki wa vyombo vya habari kuweka wakalimani wa lugha za alama katika vyombo vya habari hususani kwenye runinga kutokana na kundi hilo kukumbwa na changamoto ya kutosikia na kusababisha kutoelewa taarifa mbalimbali katika jamii.
Hayo yalisemwa jana na Katibu wa CHAVITA Mkoa wa Morogoro, Salumu Ally, alisema licha ya Serikali kutoa muongozo kwa vyombo vya habari kuweka wakalimani ili kutafsiri maneno ya vipindi na habari,bado imekua changamoto kwa baadhi ya vyombo kutotii agizo hilo.
Akizungumzia suala la kushirikishwa katika kugombea nafasi za uongozi pamoja na kupiga kura kwa watu wenye ulemavu, Salumu aliiomba Serikali na viongozi wa vyama vya siasa kuhakikisha wanaweka wakalimani wakati wa kampeni ili nao waweze kuelewa sera zinazotolewa na wagombea.
“Ningependa kusema daima kuwapo na wakalimani kwenye vyombo vya habari, pamoja na jamii kwamfano kwenye uchaguzi ili kuwasaidia viziwi kuelewa, viziwi wapewe sapoti, na wasiwe na wasiwasi na endapo Serikali itakishirikisha chama chetu itakuwa jambo zuri litakalowainua kugombea uongozi kama watu wengine,” alisema.
Alivitaka vyama vya siasa kutoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu kugombea uongozi katika nafasi mbalimbali kwani nao wana uwezo wa kushika nafasi mbalimbali za uongozi na wakafanya vizuri au hata zaidi ya wasio na ulemavu.
Mjumbe wa chama hicho, Enock Mbaga aliiomba Serikali kuweka wakalimani wa lugha za alama katika sehemu za kutolea huduma za kijamii, ikwemo hospitali, mahakamani na polisi ili kuwapa urahisi wa kupata huduma mbalimbali zinatolewa katika sehemu hizo.
“Viziwi wengi wanapenda kupiga kura, na kila kiziwi anahitaji mkalimani, bila mkalimani ni ngumu na sisi kuweka wakalimani sio rahisi,wanahitaji kulipwa fedha kwenye ujasiriamali na mambo ya msingi tunahitaji wakalimani,waliopo shuleni wanakosa mawasiliano,” alisema Mbaga.