Malima Lubasha -Musoma
JESHI la Polisi Wilaya ya Musoma mkoani Mara, limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi waliokuwa wamezingira kituo kidogo cha polisi Kariakoo kwa madai ya kumukoa muuza mkaa aliyekamatwa na idara ya misitu na kufikishwa kituoni hapo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Daniel Shilla, amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kumtaja mkazi huyo kuwa ni Mtatiro James (48) wa Mtaa wa Nyabisare Manispaa ya Musoma hivyo jeshi hilo la polisi kulazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi hao.
Alisema chanzo cha wananchi kuzingira kituo kidogo cha Polisi Kariakoo ni kile kilichodaiwa kuwa Mtatiro James amejeruhiwa kwa mapanga na askari wa Idara ya Misitu wakati wakikabiliana naye kumkamata akiwa na gunia mbili za mkaa kwenye pikipiki.
Naye Ofisa Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Ayubu Michael, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kukanusha askari wake kumjeruhi mwananchi huyo, kwamba si za kweli kwani walimpa amri ya kusimama ili kumuhoji umiliki wa mazao aliyokuwa nayo lakini kwa sehemu kubwa hakutaka kusimama kujibu hoja zao akaamua kutumia panga alilokuwa nalo mkononi kujihami.
Alisema kuwa katika kulinda usalama wao waliamua kutumia mikono yao kushika panga hilo ili kumnyang’anya lakini katika harakati za kutaka kumnyang’anya lile panga kwa wingi wao waliokuwa nao alijikuta akijijeruhi na panga hilo mwenyewe.
Aliwataka wananchi kuiacha idara ifanye kazi wanapotekeleza majukumu yao na kushirikiana nao kuzuia biashara hiyo inayiendelea mitaani kimsingi inakiuka sheria hivyo kuharibu rasilimali hiyo kwa vizazi vijavyo.
Majeruhi huyo amelazwa hospitali ya mkoa kwa matibabu akiwa chini ya ulinzi wa jeshi la polisi akipata nafuu atafikishwa mahakamani kwa hatua zaodiza kisheria.