RAYMOND MINJA IRINGA
Kampuni ya Usindikaji maziwa ya Asas mkoani Iringa imetoa msaada wa barakoa 1,000 kwa umoja wa madereva bajaji mkoani humo (UMBI) ili kujikinga na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona.
Akizungumzia msaada huo Mkurugenzi wa uzalishaji wa kampuni hiyo, Ahmed Salim amesema wameamua kusaidia kundi hilo kutokana na mchango wao mkubwa wanaoutoa katika jamii akidai wanakuta na watu mbalimbali katika majukumu yao.
“Nyie ni watu muhimu katika kusafirisha watu mbalimbali kwenda kwenye majukumu yao ya kila siku hivyo ni imani yetu kuwa barakoa hizi 1,000 zitawasaidia kwa muda na tutaendelea kushirikiana nanyi kusaidia hali ikiruhusu,” amesema mkurugenzi huyo.
Amesema kuwa mbali na barakoa kampuni hiyo imetoa vitakasa mikono, mashine ya kupulizia mwili mzima na ndoo lengo likiwa ni kusaidia kwa kurudisha kidogo wanachopata kwenye jamii ambayo kwa namna moja au nyingine inatumia malighafi za kampuni hiyo.
Akizungumzia msaada huo Mwenyekiti wa umoja huo, Norbeth Sumka amepongeza kampuni hiyo kwa kuwakumbuka madereva bajaji ambao walikuwa wanapitia changamoto ya uhaba wa vifaa hivyo.
Amesema kuwa mbali na kupewa barakoa hizo kampuni ya ASAS imekuwa ikiwaunga mkono mara kwa mara kwani iliweza kutoa ndoo na vitakasa mikono katika vituo vyote vya bajaji ili abiria waweze kutakasa mikono yao kabla ya kupanda.