29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge CCM waja juu baada ya Matiko kusema ahadi zahanati kila kijiji imekwama

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MBUNGE wa Tarime Mjini, Ester Matiko (Chadema), amewekwa mtu kati na wabunge wa CCM na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara, baada ya kudai kuwa chama tawala kimeshindwa kutekeleza ahadi yake iliyo kwenye ilani ya kujenga zahanati kila kijiji.

Mabishano hayo yalitokea wakati Matiko akichangia mjadala wa bajeti ya Tamisemi kwa mwaka 2020-2021.

Matiko wakati akichangia mara kwa mara wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walikuwa wakimpa taarifa kuhusu mambo mbalimbali.

Alisema ukipitia ilani ya CCM haikutendewa haki kwani ilieleza kila kijiji kitakuwa na zahanati, lakini hadi sasa zimejengwa zahanati 338 kati ya 12,000 ambazo ziliahidiwa.

“Hamkuitendea haki ilani ya CCM, mlisema mtahakikisha kila kijiji ama mtaa kunakuwa na zahanati, ukiangalia kwenye hotuba ya waziri kwa miaka hii wanakaribia  kabisa 338, mnasema tumechapa kazi, hadi mfikie  12,000 ni lini,” alisema Matiko.

Alisema wanakijiji wengi wamemaliza maboma ambayo Serikali iliagiza kwamba wajenge, lakini imeshindwa kumalizia hadi sasa.

“Wanakijiji wanajenga maboma, lakini nyinyi Serikali mnashindwa kuendeleza. Hamthamini  afya au utu wa Mtanzania, tunapeleka fedha kwenye vitu ambavyo sio vya muhimu, mngechukua hata trilioni 3/- tu mmalizane na hii adha,” alisema Matiko.

Wakati akiendelea kuchangia, Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga (CCM) aliomba kumpa taarifa Matiko na kudai kwamba mbunge huyo awe anatoa taarifa kwa usahihi kwani mwaka 1992 kulikuwa na hospitali ngapi na mwaka huu kuna hospitali ngapi.

“Nampongeza Ester Matiko kwa kujua taarifa za CCM, awe anatoa taarifa mwaka 92 tulikuwa na hospitali ngapi na sasa hivi tuna hospitali ngapi. Tunabadilisha mpango wetu kulingana na jinsi tunavyozaliana,” alisema Kitwanga.

Akiendelea kuchangia, Matiko alidai kwamba hawezi kupokea taarifa hiyo kwa kuwa haina tija yoyote kwani mwaka 1992 chama kilichokuwa kikiongoza ni hicho hicho.

Kauli hiyo ilisababisha Mbunge wa Hanang, Merry Nagu (CCM) naye kumpa taarifa mbunge huyo kwamba asiseme katika jimbo lake kuna kituo kimoja kwani Serikali imejenga vituo vingi vya afya katika maeneo mbalimbali.

“Namuomba mbunge asiseme maneno ambayo hayana ‘statistics’ kituo kimoja, leo tayari mimi ninavyo vinne, atasema nini, asiseme kwake, nchi nzima wamepata mambo mengi pamoja na barabara maji na madarasa, naomba sana tukubali mambo mazuri yanayofanyika,” alisema Dk. Nagu.

Akiendelea kuchangia, Matiko alisema kwamba hawezi kupokea taarifa hiyo kwani anao mfano Tarime Vijijini kuna vituo vichache vya afya.

Wakati akiendelea kuchangia, Waitara alisimama na kumpa taarifa Matiko kuwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imepeleka fedha kujenga vituo vya afya vya Mkende, Sirari na Bomali katika Jimbo la Tarime.

“Nimpe  taarifa kwamba Serikali hii ya CCM imepeleka Mkende Sh milioni 400, tumepeleka Sh milioni 500 Sirari, Bomali Sh 46, tumepeleka Sh 650 Tarime vijijini hivyo mbunge awe anatoa taarifa za kweli,” alisema Waitara.

Akiendelea kuchangia, Matiko alisema Waitara amepaniki kwani wamesema watajenga kwa kila kata, lakini wamepeleka sehemu moja tu.

Wakati akiendelea kuchangia, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson alimwelekeza Matiko kwamba asijibizane na mtu mwingine bali azungumze na yeye.

”Zungumza na mimi, usijibizane, zungumza na mimi,” alisema Naibu Spika.

Akiendelea kuchangia, Matiko alisema: ”Wabunge hawasomi, wanaenda tu, tunapongeza tu, nimesema mwanzo Tamisemi ilitakiwa kupewa fedha nyingi, leo tusipowekeza kwenye barabara hali itazidi kuwa mbaya.

“Mnajua mvua zimenyesha, bajeti hii haitoshi, tunapitisha hapa milioni 500/- lakini zinaenda milioni 200/-.

“Wananchi wanajenga maboma, lakini nyinyi hammalizii, lakini Waitara anafanya vi-ziara pale jimboni. Tuboreshe miundombinu ya kufundisha na kufundishia. Walimu hawatoshi, mmeshindwa kuajiri mnategemea elimu itaenda mbele, bila elimu tutazidi kuwa mazuzu,” alisema Matiko.

Alisema yeye amejenga madarasa kadhaa katika jimbo lake wakati sio jukumu lake ni jukumu la Serikali.

“Naomba sana mimi naweza nikaongea, lakini mimi sio jukumu langu kujenga, lakini mimi nimejenga madarasa kwa mfumo wangu wenyewe, sio wajibu wangu ule,” alisema Matiko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles