Allan Vicent
ASKARI wa Jeshi la Akiba (mgambo) wa Kijiji cha Ushokola wilayani Kaliua mkoani Tabora, wanatuhumiwa kumuua mkazi wa kijiji hicho, Juma Rajabu (40) kwa kutolipa Sh 1,000 ya mchango wa ujenzi wa choo cha Shule ya Msingi Ushokola.
Akizungumza na MTANZANIA jana Mkuu wa Wilaya ya Kauliua, Abel Busalama, alisema kuwa tukio hilo lilitokea wiki iliyopita saa 4 asubuhi.
Alisema kuwa mgambo hao ambao walitambulika kwa majina ya Moses Kiliano na Maganga Mparis wakiwa katika ukusanyi wa michango ya ujenzi wa choo kwa kila familia walifika nyumbani kwa marehemu lakini hawakumkuta.
Alisema baada ya kufika nyumbani hao walimkuta mke wa marehemu ambapo walipodai mchango wa Sh 1000, aliwambia kwamba hana fedha hizo na kumchukua hadi katika ofisi ya Ofisa Mtendaji wa Kijiji na kumuweka mahabusu hadi mume wake atakapokuja kulipa fedha hiyo.
Mkuu hiyo wa wilayan, alisema kuwa baada ya mume huyo kufika ofisini hapo alipodaiwa kiasi hicho alisema kuwa alishalipa ambapo majibu hayo hayakuwapendeza mgambo hao na kuanza kumlazimisha alipe fedha hiyo huku akimpiga.
“Mgambo walimuumiza marehemnu na walimchukua hadi Kituo cha Polisi Kaliua kuomba PF3 ili akapatiwe matibabu hospitali na baada ya kuipata walimpeleka zahanati ya mtu binafsi iitwayo Msamaria na kumwacha hapo kisha wakatokomea kusikojulikana.
“Baada ya kuona hali sio nzuri, ndugu zake waliamua kumpeleka Hospitali ya Misheni ili akapate matibabu zaidi lakini wakati juhudi za kumpatia matibabu hayo zikiendelea alifariki dunia,” alisema DC Busalama.
Ndugu wa karibu wa marehemu alilieleza gazeti hili kuwa Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani humo kwa upelelezi wa tukio hilo huku mgambo wanaotuhumiwa kumuua marehemu wakiendelea kusakwa.