26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 21, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yapeleka Sh bil 18 za elimu

simbachaweneNA RAMADHAN HASSAN, DODOMA

SERIKALI imepanga kupeleka Sh bilioni 18.77 kila mwezi kwa ajili ya kugharimia elimu bure kuanzia Januari, mwakani.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene alisema fedha hizo zitapelekwa kwa awamu ili zitumike kama ilivyokusudiwa.

Alisema katika mpango huo, Serikali itagharimia gharama zote za  mtihani wa kidato cha nne kwa wanafunzi wote, tofauti na miaka yote ambapo wanafunzi hutozwa gharama za mitihani.

Alisema fedha hizo zitatolewa moja kwa moja na Serikali kupia  Baraza la Mitihani (NECTA).

“Majukumu ya Serikali kuhusu utoaji elimu bila malipo yameelezwa katika waraka wa elimu namba 6 wa mwaka 2015, Serikali itabeba jukumu hili. Kutokana na kuwabana mafisadi tumeweza kupata fedha za kutosha.

“Serikali itatoa ruzuku ya uendeshaji wa shule Sh 10,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi na Sh 25,000 kwa mwanafunzi wa sekondari kila mwaka.

“Pia tutatoa Sh 1,500 kwa siku kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari  kwa ajili ya chakula hasa wale wanaokaa bweni,” alisema.

Alisema Serikali itatoa fedha kwa ajili ya fidia ya ada Sh 20,000 kwa kila mwanafunzi wa shule ya kutwa na Sh 70,000 kwa mwanafunzi wa sekondari kwa mwaka.

Alisema fedha za ruzuku ya uendeshaji wa shule, zitasaidia uendeshaji wa shule za bweni ikiwamo gharama za chakula, walinzi, mpishi, umeme na maji.

Aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri husika kuhakikisha fedha hizo zinafika kwa wakati na zinatumika kwa kazi iliyokusudiwa.

WAZAZI NA WALEZI

Alisema majukumu ya wazazi pamoja na mambo mengine, yatakuwa ni kununua sare za shule, vifaa vya kujifunzia, gharama za matibabu, nauli, gharama za chakula kwa wanafunzi wa shule za kutwana  kununua magodoro, shuka, vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wa bweni.

“Natoa wito  kwa viongozi wote wakiwemo wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa kusimamia utekelezaji wa elimu bila malipo,” alisema.

Aliziagiza halmashauri na mikoa ambayo haikufanya vizuri katika mitihani ya darasa la saba kujieleza sababu za kutofanya vizuri.

“Iwapo itathibitika kuna wahusika walizembea kutimiza majukumu yao, wachukuliwe hatua zinazostahili.

“Nawaagiza pia wakurugezi mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma ifikapo Februari 15, mwakani wawe wamekamilisha miundombinu ya shule ili wawewezeshe wanafunzi 12,647 waliosalia kujiunga na elimu ya sekondari wanaenda shule,” alisema.

Alizitaka kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya kuwachulia hatua za kisheria watu watakaosababisha wanafunzi kukatisha masomo kwa utoro na mimba pamoja na wale waliooa watoto wa kike.

‘’Tusifanye kazi kwa mazoea,tunatakiwa tuendane na kasi ya Rais Dk.John Magufuli ya kufanya kazi kuwasaidia wananchi hasa katika sekta ya elimu’’alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles