22.5 C
Dar es Salaam
Saturday, June 22, 2024

Contact us: [email protected]

Vilio, vurugu Dar

1bWananchi wapambana na polisi bomoabomoa

Ruth Mnkeni, Dar es Salaam

VILIO na vurugu vimetawala jijini Dar es Salaam jana wakati wa uwekaji wa alama za X katika nyumba zilizojengwa katika maeneo ya Bonde la Mto Msimbazi ambapo wananchi walipambana na Jeshi la Polisi.

Askari polisi walilazimika kutumia risasi za moto, mabomu ya machozi pamoja na magari ya maji ya kuwasha ili kutawanya wananchi waliokuwa wakipinga kuwekewa alama  hizo katika nyumba zao.

Vurugu hizo zilitokea katika maeneo ya Jangwani na Kigogo, ambapo maofisa wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na wale kutoka Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC), walishindwa kufanya kazi hiyo na kulazimika kuomba nguvu ya Jeshi la Polisi.

Kazi hiyo iliyoanza saa tatu asubuhi, ilikwama kwa muda wa saa kadhaa hadi polisi walipofanikiwa kudhibiti vurugu hizo na kutoa nafasi kwa maofisa hao kuendelea tena kuweka alama za X saa nane mchana.

Maofisa hao wa Wizara ya Ardhi pamoja na NEMC waliweza kuendelea na kazi hiyo wakiwa chini ya ulinzi wa polisi.

Wakati maofisa hao wakiendelea na kazi hiyo, liliibuka kundi la wananchi wakiwa na mabango yaliyosomeka: ‘Sadiq tupe viwanja vyetu’, ‘Magufuli bora kufa kuliko kubomolewa’ na ‘Bora mafuriko kuliko bomoabomoa’.

 

 VURUGU KIGOGO

Wakati kazi ya kuweka alama ya X ikiwa inaendelea maeneo ya Jangwani, ziliibuka vurugu kubwa za wananchi katika eneo la Kigogo, ambao walifunga barabara ya Kawawa kwa muda wa saa mbili na kuchoma matairi barabarani.

Baada ya kuchukua uamuzi huo, wananchi hao walianza kurusha mawe kwa maofisa na watu waliokuwa wakisogea kwenye eneo hilo.

Ilipotimu saa 5:40 asubuhi askari polisi walifika katika eneo hilo huku wakiwa katika magari yenye namba za usajili PT 3894 na jingine PT 3904 aina ya Toyota Land Cruiser na kuanza kuwatawanya wananchi hao kwa mabomu na risasi za moto.

Dakika chache baadaye askari hao waliongezewa nguvu kwa kuletwa wengine wakiwa katika magari yenye namba za usajili PT 3675 pamoja na gari la Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji lenye namba za usajili STK 269.

Wakizungumza na MTANZANIA, baadhi ya wakazi wa eneo hilo walieleza kusikitishwa na tukio hilo, huku wakiihoji Serikali kwamba watakwenda kuishi wapi.

“Sisi tunafunga barabara kukataa kuwekewa X katika nyumba zetu japokuwa polisi wanakuja na kurusha risasi na kutumia mabomu ya machozi, kinachotakiwa ni vyema Serikali itusikilize kwanza kwani na sisi hatukatai kuondoka ila ituonyeshe pa kwenda.

“Si halali sisi kuondolewa hapa, watu tuna familia zetu kwa kipindi hiki tunaenda wapi? Vyumba vya kukodi sasa hivi ni kuanzia Sh 70,000 kwani wanajua hawa wamebomolewa hawana pa kwenda.

“Itakumbukwa kwamba tulijenga tukiwa na Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) sasa inatugeuka kweli. Wananchi hatupingi kuhama, lakini tutengezewe mazingira mazuri ya sehemu za kuhamia,” alisema mmoja wa wananchi aliyejitambulisha kwa jina la Boniface Peter.

Pia mmoja wa wananchi hao ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini, alisema kuwa haiingii akilini Rais John Magufuli kutoa agizo wananchi wa mabondeni kubomolewa nyumba zao bila kujua kwamba wataenda kuishi wapi.

Alisema wananchi wengi wanaweza kupoteza maisha kutokana na msongo wa mawazo, kwani mtu haoni sababu ya kuishi huku familia ikiwa inamwangalia na hana pa kuanzia.

“Sisi kuhama kipindi hiki cha Serikali ya Magufuli sio mbaya, lakini ituonyeshe pa kwenda. Hii haiingii akilini kwanza tunalipa kodi serikalini kila mwaka, hatimiliki tunazo, maji yapo na huduma nyingine kama umeme je, wao hawakuyaona haya mapema leo wanaanza kutufukuza kama wakimbizi?”

“Ni heri wangeboresha miundombinu ikiwamo mifereji ya maji ili kipindi cha mvua maji yawe yanapita haraka ili kuondokana na mafuriko yanayojitokeza mara kwa mara katika jiji la Dar es Salaam,” alisema.

Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Rehema Juma, alisema kuwa Bonde la Mbuyuni ambalo lipo maeneo ya Kigogo lina zaidi ya watu 16,000 ambapo nyumba moja inaishi zaidi ya familia nne.

MTANZANIA liliona baadhi ya nyumba ambazo zitakumbwa na adha hiyo likiwamo jengo la Kanisa la Hema ya Ukombozi Kigogo.

 

KAUALI YA NEMC

 Akizungumzia bomoabomoa hiyo, Mwanasheria wa NEMC, Manchare Heche ambaye alikuwapo katika eneo la Jangwani wakati wa uwekaji alama za X, alisema ubomoaji huo utahusisha nyumba zote zilizopo katika bonde la Mto Msimbazi.

Alisema kuwa wao wameanza kuweka alama katika nyumba zote zinazohitajika kubomolewa, hivyo ni vyema watu wakaanza kuondoka mapema.

 

WATATU WAKAMATWA

Katika vurugu hizo, wananchi watatu walikamatwa, huku askari polisi wakilalamikiwa kwamba waliwafuata watu hao maeneo ya vichochoroni.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Msaidizi wa Jeshi la Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Matei Ureth, alisema waliwakamata wananchi ambao walikuwa wakihamasisha fujo wakati kazi ya uwekaji alama ya X inaendelea.

“Kwa kweli wapo watu wanane ambao tuliwakamata, lakini baada ya kuwachunguza kwa makini tuligundua kuwa wenye makosa ni watatu na ndio waliochukuliwa,” alisema Kamanda Ureth.

Mbali na hilo, alisema wananchi wanatakiwa kutambua kwamba Jeshi la Polisi halihusiki na bomoabomoa bali Wizara ya Ardhi na NEMC, na wao kazi yao ni kuimarisha usalama wa raia.

 

 KAULI YA WAZIRI

 Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, alisema wakazi milioni 3.6 watakosa makazi ambapo zaidi ya nusu ya nyumba zilizojengwa katika maeneo hatarishi zitabomolewa Dar es Salaam.

Alisema pamoja na hali hiyo awamu ya kwanza ya bomoabomoa itahusisha hekta 1,977 kuanzia eneo la Vingunguti hadi Daraja la Salander.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles