25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Prof. Lipumba: Dk. Shein anataka Wabara waandamane kumpinga

Pg 2Na Fredy Azzah, Dar es Salaam

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ameibua maswali kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na kusema kiongozi huyo anahujumu juhudi za Rais Dk. John Magufuli  za kutekeleza sera za kujenga uchumi wa viwanda na kupambana na rushwa.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za CUF Buguruni, Dar es Salaam jana, Profesa Lipumba alimmwagia sifa Rais mstaafu Jakaya Kikwete akisema kuwa alijenga hoja za kidiplomasia hali iliyosaidia nchi kupata misaada kwa kujenga miundombinu na kuimarisha sekta ya nishati.

Alisema pamoja na kwamba Dk. Magufuli anataka kuondokana na mfumo wa uchumi tegemezi katika kipindi cha mpito, ni wazi kuwa misaada inahitajika kabla ya kufikia lengo hilo.

Profesa Lipumba alisema ni vyema Dk. Shein akakubali kukamilisha mchakato wa uchaguzi wa Zanzibar wa Oktoba 25 na kumtangaza mshindi bila kusikiliza wapambe ili alinde amani ya Tanzania na kuruhusu juhudi za kuleta maendeleo ziendelee.

 

 MASWALI YA PROF. LIPUMBA KWA DK. SHEIN

 “Ni kwanini Dk. Shein anashindwa kuthamini juhudi hizo au anahitaji Watanzania bara wafanye maandamano ya kumpinga?

 “Au anataka kumuharibia Rais Magufuli asitekeleze sera zake za kupambana na rushwa na kujenga uchumi wa viwanda unaoongoza ajira na kutokomeza umasikini, bali ashughulikie matatizo ya kisiasa na kiusalama ya Zanzibar na kushutumiwa kuwa anavunja haki za binadamu?

“Anataka Watanzania wa bara tufanye maandamano ya kumshutumu kuwa anavuruga nchi na kuhujumu utekelezaji wa sera za Rais Magufuli?

“Je, Rais Shein anataka kuleta vurugu za kisiasa Zanzibar kutokana na kukataa kukamilisha mchakato wa uchaguzi wa Oktoba 25 na kumtangaza mshindi?

“Je, anataka kuwapa fursa watu wenye siasa kali inayopinga demokrasia kuhamasisha vijana Zanzibar?

“Rais Shein anataka kuharibu matunda ya diplomasia ya Rais Kikwete aliyoshiriki kuyaleta akiwa Makamu wa Rais wa Tanzania?” alihoji Profesa Lipumba.

Pamoja na hayo, Profesa Lipumba alihoji kwamba Rais Dk. Magufuli pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje, Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kikanda na Uhusiano wa Kimataifa, Balozi Dk. Augustino Mahiga, wanaweza vipi kusuluhisha migogoro ya nchi nyingine (Burundi), kama Zanzibar italipuka kwa sababu Dk. Shein kakataa matokeo?

Licha ya hali hiyo, Profesa Lipumba alihoji kama Dk. Shein yupo tayari kuharibu wasifu wake mzuri alioujenga tangu akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Jakaya Kikwete.

Profesa Lipumba alihoji pia kama uchaguzi wa Zanzibar umeharibika, kwanini kura za wabunge wa Zanzibar na Rais wa Muungano zihesabiwe ni halali wakati ulifanyika siku moja kwa kutumia daftari moja la ZEC?

 

 SIFA KWA JK

 Profesa Lipumba alisema Kikwete alifanikisha Tanzania kupata msaada wa Mpango wa Milenia (MCC), wa dola za Marekani 698, kutoka Marekani na ukagharamia miradi ya miundombinu, nishati na maji katika kipindi cha mwaka 2008-2013.

Alisema Kikwete pia alifanya maandalizi ya kupata dola milioni 472.8 za awamu ya pili ya MCC, ambazo zilikuwa zifanikishe kupata umeme wa uhakika nchini.

 

 MIRADI ITAKAYOKWAMA

 “Msaada huu wa pili unajumuisha dola milioni 58.6 zitakazoimarisha ZECO (Shirika la Umeme Zanzibar) na sekta ya umeme Zanzibar. Sasa uko hatarini kusambaratika ikiwa maamuzi ya wananchi wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 hayataheshimiwa,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema fedha hizo ambazo tayari Bodi ya MCC imesitisha kuzitoa, zilitarajiwa pia kutekeleza mpango wa Serikali wa  kurekebisha sekta ya umeme nchini na kuunganishia zaidi ya kaya 300,000 nishati hiyo.

“Msaada huu pia ulitarajia kurekebisha sekta ya umeme Zanzibar na kuanzisha ufuaji wa umeme wa megawati 5 wa kutumia jua au upepo,” alisema.

Alisema kushindwa kuheshimu maamuzi ya wananchi wa Zanzibar, kunafanya Tanzania ikose misaada hiyo ambayo ingesaidia kuinua sekta ya nishati nchini.

Kauli hiyo ya Profesa Lipumba imekuja siku moja baada ya CUF kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Ismail Jussa Ladhu, kusema kuwa wataendelea kusimamia na kulinda chaguo la Wazanzibari katika Uchaguzi wa Rais wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Pamoja na hali hiyo, CUF imesema bado inatoa nafasi kwa Rais Magufuli kwa jitihada anazozifanya katika kuupatia ufumbuzi wa haraka mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar ambao matokeo yake yalifutwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha.

Jussa alisema pamoja na kile alichokiita hila amewataka wananchi kupuuza taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Waride Bakari Jabu, kuhusu kurudiwa kwa uchaguzi huo.

Alisema taarifa ya Waride ni sawa na kufunika kombe kutokana na maswali wanayoulizwa na wanachama wao juu ya kutumia mabilioni ya fedha, lakini wakashindwa vibaya kwenye uchaguzi.

Oktoba 28, mwaka huu, Jecha alitangaza kufuta uchaguzi wa Zanzibar akisema haukuwa huru na wa haki.

Hata hivyo,aliyekuwa mgombea urais kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema hakubaliani na uamuzi huo na kuitaka ZEC iendelee na kazi yake ya uhakiki wa matokeo ya uchaguzi na kisha kutangaza mshindi.

Maalim Seif alisema CUF imeonekana wazi kwamba ni mshindi wa uchaguzi wa rais pamoja na majimbo yote 18 ya Pemba na mengine tisa ya Unguja.

 

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles