BAADA ya kupatikana washindi wa Miss Albino Kanda ya Mashariki na Kaskazini, kwa sasa shindano hilo linatarajiwa kufanyika Kanda ya Ziwa mwishoni mwa mwezi ujao jijini Mwanza ikiwa ni harakati za kuendelea kumsaka Miss Albino Tanzania 2016.
Mratibu wa shindano hilo, Alexander Matowo, aliliambia MTANZANIA jana kuwa maandalizi kwa ajili ya kumpata mshindi huyo yanaendelea ambapo tarehe na ukumbi vitawekwa wazi mwishoni mwa wiki hii.
Washindi waliopatikana hadi sasa ni Priscilla Samweli wa Kanda ya Mashariki mkazi wa Chanika jijini Dar es Salaam na Eveline Felixoiso wa Kanda ya Kaskazini mkazi wa Boma mkoani Arusha.
“Shirika lisilo la kiserikali la Save Vulnerable Foundation (SVF) ndilo linaendesha shindano hilo na lengo ni kutambua thamani ya watu wenye ulemavu wa ngozi ambao wamekuwa wakiuawa kikatili na watu wenye imani potofu na muda mrefu wamekuwa wakitengwa katika jamii hasa kwenye mashindano ya kuwasaka warembo wa Tanzania, hivyo tumeona nao tuwaandalie shindano lao,” alisema Matowo.