Na Grace Shitundu , Dar es Salaam BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limewataka wawekezaji wa hoteli zilizopo pembezoni mwa bahari kuacha kuwatoza wananchi fedha za kiingilio wanapokwenda katika fukwe hizo kupunga upepo au kuogelea.
Tamko hilo limekuja kutokana na baadhi ya hoteli katika Jiji la Dar es Salaam kubainika kutoza fedha kuanzia Sh 10,000 hadi 40,000 kwa mtu mmoja kama gharama za kuogelea.
Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA umebaini kuwa wamiliki wa hoteli hizo wamekuwa wakifanya hivyo katika sikukuu mbalimbali na zile za mwisho wa mwaka, jambo ambalo limekuwa likileta kero kwa jamii.
Akizungumzia suala hilo Mwanasheria wa NEMC, Manchari Heche, alisema kwa mujibu wa sheria, fukwe zote ni mali ya umma, hivyo wananchi hawatakiwi kutozwa fedha wakati wanapokwenda kutembea au kuogelea.
“Kifungu cha 57 cha sheria ya mazingira kimeweka ukomo wa mpaka wa kila kiwanja kilichopo karibu na ufukwe.
“Beach (fukwe) zote ni mali ya umma kwa sababu kuna mipaka yake, hivyo kitendo cha kuwatoza wananchi fedha za kuingia katika fukwe hizo ni kosa kisheria na wanaofanya hivyo wanapaswa kuacha mara moja,”alisema Heche.
Kuhusu ujenzi karibu na fukwe hizo, Heche alisema wawekezaji wa hoteli wanapaswa kujenga umbali wa mita 60 kutoka katika ukingo wa bahari na kama kuna mwekezaji aliyezidisha umbali huo anapaswa kubomoa mwenyewe kabla hajachukuliwa hatua za kisheria.
“Wale waliokiuka na kujenga hadi katika eneo la bahari waanze sasa kuboboa wenyewe kwa kuwa zoezi la bomoabomoa nao litawahusu”, alisema.
Wiki iliyopita Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais(Muungano na Mazingira), January Makamba alitoa taarifa ya Serikali kwamba sheria hiyo ya NEMC itatekelezwa kwa ukamilifu wake.
Alisema operesheni ya kuwaondoa watu wanaoishi na kufanya shughuli kwenye maeneo ya kingo za mito na maziwa, fukwe za bahari, maeneo oevu na maeneo ya wazi imeshaaanza.
Katika Jiji la Dar es Salaam, zoezi la kuwaondoa wananchi waliojenga mabondeni lilianza rasmi Desemba 17 mwaka huu na kusimama kwa muda ambapo litaendelea Januari 5 mwakani huku, zaidi ya nyumba 353 zikiwa tayari zimebolewa na nyingine zaidi ya 8,000 zinatarajiwa kubomolewa.