26.8 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Mawaziri waja na mikakati mizito

mtz1NA FREDY AZZAH, DAR ES SALAAM

MAWAZIRI wapya walioteuliwa wiki iliyopita na Rais Dk. John Magufuli, wameapishwa na kueleza mikakati yao.

Wakizungumza jana jijini Dar es Salaam baada ya kuapishwa, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, amewaahidi Watanzania kupata elimu bora, huku Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, akitangaza kiama kwa wakwepa kodi.

 

PROFESA NDALICHAKO

Profesa Ndalichako alisema kipaumbe chake cha kwanza ni kuhakikisha elimu bora inapatikana kwa kila mtoto wa Kitanzania.

Alisema atatumia nafasi aliyonayo kuhakikisha mtoto anapelekwa shule na kupata elimu ambayo jamii yake inaitegemea.

Kutokana na mikakati yake hiyo, Profesa Ndalichako aliwaomba Watanzania wampe ushirikiano katika kufikia azma hiyo.

Alisema ili kufikia lengo hilo ni lazima shule ziwe kwenye mazingira mazuri ikiwamo kuhakikisha wanafunzi wanakaa katika madawati, na kuwataka watendaji kuhakikisha suala la kukaa chini linakuwa historia.

“Suala jingine kwa shule binafsi waangalie namna ya kupunguza michango isiyo ya lazima, kwa mfano ni kwanini uwaambie wazazi wachangie fedha ya kujenga madarasa? Wewe unaomba kibali cha shule na kupewa alafu bado unataka wazazi wachangie hela ya madarasa,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wamiliki wa shule binafsi kuacha tabia ya kutoza ada kubwa tofauti na wanayoweka kwenye fomu ya mwanafunzi kujiunga na shule husika.

“Unakuta wengine kwenye fomu wamesema ada ni Sh milioni moja, mtoto akifika shuleni anaambiwa alipe Sh milioni mbili. Nawataka watendaji wanaotoa ithibati kwa shule na vyuo binafsi waangalie sana hili,” alisema Profesa Ndalichako.

Aliwataka watendaji wa wizara yake na sekta ya elimu kwa ujumla kuhakikisha wanajipanga ili kuendana na kasi yake kwa kuwa yeye tayari yuko tayari kuendana na kasi ya Rais Magufuli.

 

  1. MPANGO

Kwa upande wake, Dk. Mpango alisema wizara yake itahakikisha kila anayepaswa kulipa kodi analipa kama inavyotakiwa.

Alisema kwa siku 27 alizokaa Mamkala ya Mapato Tanzania (TRA), amejifunza mengi ambayo yatamsaidia kwenye utendaji kazi zake.

“Tutafanya kila liwezekanalo ili wanaokwepa kodi halali tuwabane kama mlivyoona kwa siku 27 nilizokaa TRA, lakini pia lazima turekebishe mfumo wa kodi na kuondoa zile kodi ambazo ni kero na mfumo uwe rafiki kwa wafanyabiashara, vinginevyo tutaendelea kuwabana walewale wadogo kila siku,” alisema Dk. Mpango.

Alisema TRA inaendelea kukusanya kodi na kwa mwezi Desemba lengo ni kukusanya Sh trilioni 1.3.

“Kabla ya sikukuu wakati naondoka tulikuwa sehemu nzuri tu kwenye kufikia lengo letu,” alisema.

Kuhusu kuendela kutegemea wahisani, alisema lazima uchumi ukuzwe ili miaka 54 ya Uhuru taifa liweze kujiendesha.

“Inabidi tupambane tuache kuendelea kutegemea misaada, mimi nilikuwa naongozana na mawaziri walionitangulia wakati wa kuomba misaada, si kitu kizuri kabisa, kwa kweli inakera,” alisema Dk. Mpango.

 

PROF. MAGHEMBE

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alisema kipaumbele chake kikubwa kitakuwa ni kupambana na ujangili nchini

“Niwaambie majangili sasa wakafanye kazi nyingine ama wakae nyumbani, kiama kinakuja huko, jambo la pili nitakaloshughulikia ni misitu, kuitunza na kupambana na usafirishaji wa magogo na ukataji wa mkaa,” alisema Profesa Maghembe.

Alisema kuwa atasimamia kwa uhakika maliasili za Watanzania kwa sababu mambo ya maliasili ndiyo eneo alilobobea kwenye usomi wake.

“Tutajitahidi pia kutangaza utalii na kuongeza mapato ya sekta hii kama tulivyofanya kwenye miaka ya 2006 hadi 2008, tuliongeza bei za vitalu na ada kwa mnyama mmoja mmoja anayewindwa,” alisema Profesa Maghembe.

 

PROFESA MBARAWA

Naye Waziri ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema miundombinu ndiyo inajenga uchumi wa nchi, hivyo atafanya kila awezalo kuhakikisha inakuwa bora.

“Sikuchaguliwa kwa makosa kuja kwenye hii wizara, uchukuzi, ujenzi na mawasiliano ndiyo uti wa mgongo wa uchumi, nitahakikisha ujenzi wa reli ya kati ya kiwango cha kisasa ‘Standard Gauge’ unarudi kwenye mstari na kuanza haraka,” alisema Profesa Mbarawa.

Mawaziri wengine walioapishwa jana ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni.

Desemba 23, mwaka huu  Rais Magufuli alimalizia viporo kwa kuteua mawaziri wanne kuziba nafasi zilizokuwa wazi na akamuhamisha waziri mmoja na kumteua naibu waziri mmoja, hatua iliyofanya Baraza lake la Mawaziri kuwa na mawaziri na manaibu 35 tofauti na alivyosema watakuwa 34.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles