Na Mwandishi wetu, Kilimanjaro.
KAIMU Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi (Kibong’oto), DK Riziki Kisongo, amesema tafiti za magonjwa ambuzuki kutoka hospitalini hapo, zimesaidia Shirika la Afya Duniani (W.H.O) kubadilisha miongozo ya kutibu na kugundua vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu (TB).
Akiwasilisha taarifa ya hospitali hiyo kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ukimwi, Madawa ya Kulevya na Kifuaa Kikuu, Dk Kisongo alisema wana machapisho 50 ya kisayansi mbayo yamechapishwa kwenye majarida ya kimataifa.
Alisema kati ya machapisho hayo, mawili yamechangia kwenye kubadilisha miongozo ya kutibu na kugundua vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu,” alisema Dk Kisongo.
“Mwaka 2009 ilikuwa inachukua siku 392 ili mtu kugundulika ana ugonjwa wa kifua kikuu toka aende hospitali, kupitia watafiti tuliweza kutengeneza miongozo ambayo ilitoa dira ya kuwa na haja ya kuwa na vipimo vipya ambavyo vingepunguza muda wa kugundua mgonjwa wa kifua kikuu.
“Miongozo imesaidia kuja kwa vipimo vya kisasa vya ugonjwa wa kifua kikuu ambavyo zinachukua masaa mawili na nusu kufanya vipimo vya ugonjwa wa kifua kikuu,” alisema Dk. Riziki.
Alisema pia kupitia maandiko yao, sasa wagonjwa wanatibiwa kwa vidongo badala ya sindano.
“Tiba ya ugonjwa wa kifua kikuu ilikuwa ni kwa njia ya sindano kwa muda wa miezi nane, utafiti ulivyofanyika hapa ilionekana asilimia 47 ya wagonjwa walikuwa wanapata matatizo ya usikivu, kwa kuchapisha maandiko hayo ilisadia kubadili tiba ya ugonjwa huo ambapo hadi hivi sasa tiba inatolewa kwa vidonge,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Leonard Subi, aliesema Tanzania ni mojawapo ya nchi inayofanya vizuri kwenye matibabu ya TB.
Alisema hadi hivi sasa ina vituo 145 vya matibabu ya kifua kikuu sugu nchi nzima, tofauti na awali ambapo ilikuwa na hospitali ya Kibong’oto pekee.
“Lengo la kuwa na Hospitali ya Kibong’oto si kwa ajili ya kutoa tiba pekee bali wanatakiwa kubobea kwenye tafiti, tiba na matokeo chanya kwa taifa na dunia kwa ujumla” alisema Dk. Subi.
Alisema Wizara ya Afya imeiongezea hospitali hiyo uwezo wa kushughulikia magonjwa yote ambukizi, tafiti na ufuatiliaji.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi, Madawa ya Kulevya na Kifua Kikuu, Oscar Mukasa, alitaka hospitali hiyo kuongeze juhudi zaidi na kuja na tafiti nyingi zaidi zitakazo saidia katika kupata tiba ya ugonjwa huo ambao bado ni tatizo kwa Watanzania.