ROME, ITALIA
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis hataonekana hadharani ili kuzuia kukutana na mikusanyiko ya watu inayofika kumwona.
Hatua hiyo imekuja wakati maambukizi na vifo vilivyotokana na virusi vya corona nchini Italia vikiwa juu kuliko nchi nyingine yeyote duniani baada ya China.
Inaelezwa kuwa kwa sasa kiongozi huyo wa kiroho ataendesha shughuli zake nyingi ikiwa ni pamoja na kuongoza ibada kwa njia ya video kupitia mtandao wa intaneti.
Shughuli hiyo ataifanya kutoka ndani ya Vatican kwa sababu ya maambukizi ya virusi vya corona nchini Italia.
Vatican pia imesema kuwa Papa hatatumia utaratibu wa kuzungumza na mkusanyiko wa watu kupitia dirisha linalotazama kanisa la Mtakatifu Petro mjini Roma ambalo ni kubwa kuliko yote duniani.
Zaidi hatakuwa na mikutano mingine katika eneo hilo au siku ya Jumatano.
Papa mwenye umri wa miaka 83 hajafanya misa hiyo ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi chote cha upapa wake.
Pamoja na hayo Vatican inasema kiongozi huyo anasumbuliwa tu na baridi ambayo haina dalili zinazohusiana na magonjwa mengine.
Wakati kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani, akichukua uamuzi huo, idadi ya watu waliokufa kwa virusi vya corona nchini Italia imepanda hadi kufikia 197 baada ya ongezeka la vifo vingi kila siku tangu maambukizi hayo yazuke.
Maofisa wanasema watu 49 wamekufa nchini humo ndani ya saa 24, wakati kukiwa na maambukizi ya zaidi ya kesi 4,600 zilizoripotiwa.
Nchi hiyo sasa imeripoti vifo vingi nje ya China, ambako virusi hivyo vilizuka mwezi Desemba katika mji wake wa Wuhan ulioko katika jimbo la Hubei.
Shirika la Afya Duniani la (WHO) linasema karibu watu 100,000 duniani kote wameambukizwa virusi hivyo huku zaidi ya 3,000 wakifa wengi wao wakiwa ni kutoka China.