AVELINE KITOMARY – DAR ES SALAAM
Daktari Bingwa wa Upasuaji Mifupa na Magonjwa ya Ajali kutoka Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI), Dk. Kennedy Nchimbi amesema binadamu huzaliwa akiwa na mifupa 300 lakini anapokuwa mtu mzima huungana na kuwa 206
Dk. Nchimbi amesema baadhi ya mifupa hiyo kuungana na kutengeneza mifupa mikubwa.
Dk. Nchimbi amesema ukomavu wa mifupa (Ossifications), kwa kawaida binadamu anapokuwa mtu mzima wa miaka 25 mifupa hiyo huungana kwani anapokuwa mdogo mifupa ina kuwa imeachana hivyo anavyozidi kukua ndivyo inavyoungana.
Amesema kuna sehemu mifupa inakuwa haijafunga hivyo ikihesabiwa inakuwa mingi zaidi na baadae zinaungana kwa kuwa ni za ukuaji ndio maana hurefuka.
“Zaidi ya nusu ya mifupa ya mwili wa binadamu ipo kwenye mikono na miguu na kati ya mifupa 206 mifupa 106 ipo kwenye mikono na miguu,” amesema Dk. Nchimbi.
Aidha ameeleza kwamba sehemu ambazo zinagawanyika kabla ya kukomaa zinaruhusu kukua (Growth plates epiphyceal plate), mfano mfupa wa paja kabla ya miaka 25 binadamu wa kawaida mfupa huo unaweza kuwa na sehemu tatu hadi nne tofauti lakini ukubwani huonekana mmoja tu.
“Ndio maana hata mtoto anapozaliwa fuvu la kichwa unaweza kulibana na huwezi kufanya hivyo baada ya kukomaa hata akina mama wanaopitiliza siku za kujifungua yaani wiki 40, hawezi kujifungua kwa njia ya kawaida ina kuwa ni shida,”namesema.