Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amemwagiza Mkurugenzi wa Elimu Msingi Tamisemi, Julius Nestory kupeleka walimu Shule ya Msingi Chiwondo iliyopo nje kidogo ya Jiji la Dodoma, kutokana na kuwa na walimu wawili tu.
Maagizo hayo aliyatoa jana jijini hapa wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika shule hiyo ambayo imejengwa na Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde (CCM).
Jafo alitoa agizo hilo baada ya Ofisa Elimu Msingi Wilaya ya Dodoma, Joseph Mabeyo na Diwani wa Kata ya Nala, Brison Eliya (CCM), kumweleza kuwa shule hiyo ina walimu wawili tu.
Kutokana na maombi hayo, Jafo alimwelekeza mkurugenzi huyo ambaye aliongozana naye, hadi ifikapo mwakani katika ajira mpya walimu wawe wamepelekwa katika shule hiyo.
Pia aliagiza hadi mwakani shule hiyo iwe imesajiliwa na ianze kutumika kama shule rasmi tofauti na sasa ambapo ni shule shikizi kutokana na Shule ya Msingi Chihoni kuwa mbali.
“Nakuagiza Mkurugenzi wa Elimu Msingi ulete madarasa mawili hapa na mwakani shule hii iwe imesajiliwa na iwe imeongezewa walimu ili hawa watoto wasitembee tena umbali mrefu,” alisema Jafo.
Kwa upande wake, Mavunde alisema wakati wa kampeni mwaka 2015, aliwaahidi wananchi atahakikisha anasimamia ujenzi wa shule mpya ili kupunguza adha kwa wanafunzi kutembea umbali mrefu.
Alisema aliwaahidi kwamba atawajengea shule na wananchi walidai kwamba wamekuwa wakiahidiwa hivyo na wagombea, lakini baada ya hapo wamekuwa hawarudi tena.
“Niliona nina deni kubwa sana, nilipochaguliwa baada ya wiki tatu nilirudi na nikaanza kuchimba msingi mwenyewe wa kujenga hii shule, nilianza kujenga madarasa mawili na ofisi, nafurahi kuwaambia leo nakabidhi madarasa zaidi ya sita,” alisema Mavunde.
Pia, alisema sababu ya kumwalika Jafo kuweka jiwe la msingi ni kutokana na wananchi hao kudai kwamba tangu nchi imepata uhuru hakuna waziri ambaye amewahi kukanyaga katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge alimpongeza mbunge huyo kwa kujenga shule hiyo huku akiwataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawapa malezi bora watoto wao ili wasiwasumbue walimu.