Leonard Mang’oha -Dar es salaam
WANAFUNZI 20 wa darasa la tano Shule ya Msingi Butiama ‘B’ wilayani Butiama, Mkoa wa Mara, wanadaiwa kuanguka wakati wakikimbia kutoka darasani kwa madai ya kuona watu wa ajabu.
Chanzo cha kuaminika kutoka eneo hilo, kililiambia MTANZANIA jana kuwa tukio hilo lilitokea kati ya saa 3:00 na saa 4 asubuhi wakati watoto hao wakiwa darasani ambapo wasichana 20 ndio walioanguka na kupelekwa hospitali ya wilaya kwa matibabu.
Kwamba kutokana na tukio hilo, uongozi wa shule uliamua kusitisha masomo kwa siku ya jana taarifa ambazo zilithibitishwa na Ofisa Elimu wa Wilaya.
Akizungumza na MTANZANIA kwa simu, mmoja wa wanafunzi katika darasa hilo ambaye jina lake linahifadhiwa, alidai kuwa wakiwa darasani walitokea watu wawili wa ajabu wenye mwonekano wa kiume wakiwa wamevaa nguo nyeusi.
“Tulivyowaona tukakimbia kuwaambia walimu, lakini walivyokwenda hawakuwaona,” alisema mwanafunzi huyo.
Gazeti hili lilimtafuta Ofisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Butiama, Joseph Omary, ambaye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, huku akidai kuwa si tukio ambalo mtu anaweza kuelezwa akalielewa kwa urahisi.
“Ndiyo, tukio hilo limetokea na hapa tunafanya kikao, lakini kwa ‘scenario’ hii hakuna tunachoweza tukasimulia ukakielewa, ‘it’s much better’ ungekuwapo hapa. Watoto wamepiga tu kelele kwamba wanawaona watu, basi kelele imekuwa kubwa tumeamua kuahirisha masomo na sasa tuna kikao,” alisema Omary.
Mwenyekiti wa Kamati ya shule hiyo, Nelson Mkirya, alisema kuwa wanatarajia kukutana leo na wazazi ili kujadili kuhusu tukio hilo pamoja na mpango wa kuwezesha wanafunzi kupata chakula shuleni.
“Tutakutana kujadili kuhusu tatizo lililojitokeza na kuhusu watoto kupewa chakula shuleni, lakini pia tutakuwa na ajenda nyingine ambazo kesho tutakufahamisha baada ya kikao,” alisema Mkirya.