24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Rugemarila amtaka DPP amuondoe kwenye kesi

KULWA MZEE – DAR ES SALAAM

Mfanyabiashara James Rugemarila, ametoa notisi kwa taasisi nyeti tisa akimtaka Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga amuondoe kwenye kesi ya uhujumu uchumi na asipofanya hivyo atawasilisha hoja rasmi za kuondolewa katika kesi hiyo.

Mshtakiwa huyo ametoa taarifa hiyo leo Alhamisi Februari 13, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon aliiarifu mahakama kwamba upelelezi unaendelea na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa na baada ya kusema hayo, Rugemarila alinyoosha mkono akiomba kuzungumza na Hakimu Shaidi akamruhusu.

“Mheshimiwa hakimu nilitoa notisi sehemu mbalimbali ikiwemo kwa DPP na imepokelewa, nilitegemea kuachiwa leo kwa kuondolewa katika shauri hili.

“Nilitegemea leo Jamhuri waje na ufafanuzi juu ya barua niliyoandika kuhusu Benki ya Standard Chartered kukwepa kodi, sheria haitekelezwi, jana nimetoa notisi na kuisambaza na imepokelewa kote, ” amedai Rugemarila.

Amedai miongoni mwa taasisi alizopeleka notisi ni katika ofisi ya DPP, DCI, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Mkurugenzi wa Takukuru, Gavana wa Benki Kuu, Kamishna TRA, Wakili Mkuu wa Serikali na Kamishna wa Magereza.

Rugemarila ambaye ni Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Harbinder Sing Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa PAP, wanadaiwa kutenda makosa hayo jijini Dar es Salaam na nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha, miongoni mwa mashtaka hayo yapo ya kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi na kutoa nyaraka za kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27 za Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles