Asha Bani
Serikali imesema taasisi za mafunzo na wadau wa sekta ya utalii wanatakiwa kufanya kazi kwa pamoja ili kutatua changamto zilizopo ikiwemo nguvu kazi yenye weledi na ufanisi wa kutosha katika tasnia hiyo.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha wakati wa kufunga kongamano la kimataifa la kuunganisha wanataaluma na wadau wa sekta ya Utalii na Ukarimu ambapo amesema ushindani katika soko ni mkubwa hivyo kunahitajika maandalizi mazuri ya rasilimali watu ili kuweza kushindana katika soko la dunia.
Amesema utalii ni moja ya sekta inayolipatia taifa fedha za kigeni akitolea mfano katika kipindi cha mwaka jana nchi ilipata fedha za kigeni Dola milioni 2.4 kutokana na utalii na kusema kukiwa na nguvu kazi yenye weledi na ufanisi wa kutosha nchi itaneemeka kupitia sekta hiyo.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa kwa sasa Taifa linatoa kipaumbele katika kuimarisha viwanda ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuandaa nguvu kazi, hivyo ni vizuri kukawa na mfumo wa mafunzo pacha kati ya taasisi za mafunzo na wamiliki wa viwanda.
Naye Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dkt. Shogo Mlozi amesema kwa kushirikiana na vyuo vingine vinavyotoa mafunzo ya utalii wataendelea kuimarisha mpango wa utoaji mafunzo kwa kufanya kazi karibu na watoa huduma ili kupata nguvu kazi yenye weledi na ujuzi.
Kwa upande wake mshiriki wa kongamano hilo kutoka VETA makao makuu, Happiness Salema amesema ni vizuri kukawa na makongamano ya aina hii kwa kuwa yanawaleta pamoja watoa mafunzo na wamiliki wa viwanda, jambo ambalo linasaidia kuona changamoto zilizopo na kuweka mkakati kwani nchi zilizoendelea zinatumia mfumo huu katika kutoa mafunzo.