Theresia Gasper – Dar es Salaam
KOCHA Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, amesema kikosi chake hicho bado hakijaukosha moyo wake kutokana na kupata ushindi wa mabao kiduchu.
Akizungumza baada ya mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Ruvu Shooting kumalizika juzi na Yanga kushinda bao 1-0 lililofunga na straika David Molinga, kocha huyo raia wa Ubelgiji anaamini washambuliaji wake wakiongeza umakini, timu yake itashinda kwa idadi kubwa ya mabao kwenye michezo yao.
Alitolea mfano kwa kusema walistahili kupata ushindi mkubwa zaidi katika mchezo wao na Shooting, kutokana na kutengeneza nafasi nyingi ambazo hata hivyo hawakuweza kuzigeuza kuwa mabao.
“Tumepata ushindi lakini sio ninaoutaka mimi, bado safu yangu ya ushambuliaji ina kosa umakini, licha ya timu kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, tatozo lipo kwenye umaliziaji.
“Nina kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha tatizo hilo linaondoka na timu inashinda mabao ya kutosha,” alisema.
Alisema anahitaji timu yake ipate mabao mengi dhidi ya wapinzani wao, ukizingatia hakuna mechi rahisi miongoni mwa timu wanazokutana nazo katika ligi hiyo.
Hata hivyo, Eymael hakusita kumwagia sifa mlinda mlango wa Ruvu Shooting, Mohamed Mkaka aliyesimama langoni kwenye mchezo huo kwa kuokoa michomo mingi ya hatari iliyoelekezwa kwao na washambuliaji wake.
“Tulitakiwa kushinda mabao hata zaidi ya matatu, hata hivyo nampongeza kipa wa Ruvu(Makaka) kwani aliweza kuokoa mashuti ya hatari yaliyopigwa na wachezaji wangu na kufanya tupate ushindi wa bao 1-0,” alisema.
Katika mchezo huo, Makaka aliokoa mipira miwili ya hatari ya Molinga na mmoja wa Yikpe Gislain ambayo kama si uhodari wake ingekuwa mabao.
Washambuliaji hao wawili ambao wamekuwa wakianza kwa kupokezana, kwa sasa ndio tegemeo katika kikosi cha Yanga, ambapo Molinga amefunga mabao saba, huku Yikpe alisajiliwa dirisha dogo akifunga bao moja.
Yanga inakamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Ku, ikijikusanyia pointi 37, katika michezo 18 iliyocheza, ikishinda11, sare tatu na kupoteza michezo minne.