30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Spika aichana vipande hotuba ya Trump

Washington, Marekani

MGAWANYIKO umedhihirika katika anga ya kisiasa Marekani wakati Rais Donald Trump alipokuwa akitoa hotuba ya kila mwaka mbele ya Bunge la Congress, huku mchakato wa kumwondoa madakarani ukikaribia kumalizika.

Wakati Trump alipopanda kwenye jukwaa kutoa hotuba yake kwa taifa, alimpuuza na kukataa kumpa mkono Spika wa Baraza la Wawakilishi katika Bunge la Congress, Nancy Pelosi ambaye alikuwa amemnyooshea mkono.

Hatua hiyo ya Rais Trump kususia mkono wa Pelosi na spika huyo kumjibu kwa kuichana hotuba yake, ni baadhi tu ya vitimbi vilivyodhihirisha mgawanyiko mkali wa kisiasa nchini Marekani, wakati Trump alipotoa hotuba kuhusu hali ya nchi.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Trump kukutana uso kwa uso na Pelosi ambaye ni hasimu wake mkuu wa kisiasa anayeongoza mchakato wa Wademocrat wa kutaka kumwondoa madarakani.

Katika hotuba yake, Trump alikituhumu Chama cha Democrat kwa kupanga kuwalazimisha walipakodi wa Marekani kutoa huduma ya afya ya bure kwa wahamiaji wasio na nyaraka. Pelosi alionekana mara mbili akisema: “Sio kweli.”

Pelosi, ambaye ni kinara wa chama cha upinzani cha Democrat, alionekana mwenye hasira wakati wa hotuba ya Trump ambapo alichana vipande vipande nakala ya hotuba hiyo na kuitupa mezani.

Tofauti na ilivyozoeleka kuwa hotuba ya rais wa Marekani kuhusu hali ya nchi ni muda wa maridhiano kisiasa, mazingira katika kikao cha Congress kilichowaleta pamoja wajumbe wa baraza la wawakilishi na maseneta yaliakisi mpasuko mkali wa kisiasa muda wote wa saa moja na dakika 18 wa hotuba ya Trump.

Zoezi zima lilianza vibaya pale Rais Trump alipokataa kuupokea mkono alionyooshewa na Pelosi na kuuacha ukining’inia hewani.

Na lilimalizika kwa hatua ya Pelosi kumjibu Trump mtindo wa jino kwa jino, alipochana vipande vipande nakala ya hotuba ya Trump aliyokuwa amekabidhiwa, mara tu Trump alipomaliza kuzungumza.

Trump ambaye hakutaja kadhia hiyo ya mpango wa kumuondoa madarakani, mwanzoni mwa hotuba yake alikuwa akishangiliwa mara kwa mara na wabunge wa chama chake cha Republican.

Rais Trump alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake kwa majigambo, ya namna alivyofanikiwa kuukarabati uchumi wa Marekani na hadhi ya nchi hiyo, ambavyo amedai vilikuwa vimewekwa rehani na watangulizi wake.

”Miaka ya uozo wa kiuchumi imekwisha. Siku za Marekani kuhujumiwa kiuchumi na kukejliwa na mataifa mengine tumeziacha nyuma. Tumeipa pia kisogo mienendo ya kuvunja ahadi, na kutafuta visingizio vya kumomonyoka kwa uchumi, nguvu na fahari ya Marekani. Tumevunjilia mbali mitazamo ya kwamba Marekani inadidimia,” alisema Trump.

Masuala mengine aliyoyamulika Trump katika hotuba yake, ni mikubaliano ya kibiashara kati ya China, na mengine ya eneo huria la kibiashara katika nchi za Amerika Kaskazini, akisema hayo ni mafanikio makubwa ambayo yatarejesha maelefu ya viwanda nchini Marekani.

Alizungumzia pia sera za kupunguza kodi na kumaliza kuhusika kwa majeshi ya Marekani katika mizozo ya Mashariki ya Kati, kama ushahidi wa kutimiza ahadi alizozitoa kwa wapiga kura.

Hotuba yake ilishangiliwa mara kwa mara na wabunge wa chama chake cha Republican waliosimama kumpigia makofi, huku wademocrat wakibakia katika viti vyao, baadhi wakizomea, na wengine hata kutoka nje.

Trump ambaye baadaye, baada ya hotuba yake ya jana anatarajiwa kuondolewa katika kesi anayoshtakiwa na wademocrat kwa tuhuma za matumizi mabaya ya wadhfa wake, hata mara moja hakuitaja kesi hiyo katika hotuba yake.

Baraza la Seneti, ambalo linadhibitiwa na Warepublican, lilitarajiwa kupiga kura kuhusu iwapo Trump ataondolewa ofisini au la, ikiwa ni muda mfupi baada ya hotuba yake kwa Taifa.

Inatazamiwa kuwa Trump hataondolewa madarakani kwani Warepublican 53 katika baraza hilo wameonekana kupinga wazi mchakato huo wa Wademokrat.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles