Winfrida Mtoi – Dar es Salaam
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba leo wanatarajia kushuka dimbani kuumana na Namungo, mchezo wa ligi hiyo utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba inayonolewa na Mbelgiji Sven Vandenbroeck, itaingia uwanjani ikitoka kuichapa Mwadui mabao 2-1, katika mchezo wa michuano ya Kombe la Shirikisho ya Soka Tanzania (ASFC).
Ushindi dhidi ya Mwadui uliipeleka Simba hatua ya 16 bora ya ASFC.
Wekundu hao wa Msimbazi, wamekuwa na mwendelezo mzuri wa kupata matokeo ya ushindi katika michezo yao ya Ligi Kuu, tangu Sven alipokabidhiwa jukumu la kuwanoa, akirithi mikoba ya Patrick Aussems aliyetimuliwa.
Simba tangu ilipotoa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Watani wao Yanga,wamekuwa na uchu wa pointi tatu kwani hawajapoteza mchezo.
Mechi mbili za mwisho za Simba za Ligi Kuu, iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbao FC, kabla ya kuilaza Alliance mabao 4-1.
Matokeo hayo yameifanya kuendelea kukaa kileleni wakikusanya pointi 41, zilizotokana na michezo 16, wakishinda 13, sare mbili na kupoteza mmoja.
Akizungumzia mchezo wao wa leo, Sven alisema kiwango kinachoonyeshwa na wachezaji wake kinampa tumaini la kuendelea kufanya vizuri katika ligi hiyo.
Alisema hata hivyo upo upungufu kidogo katika baadhi ya maeneo ya kikosi chake, lakini ameendelea kuyarekebisha ili kupata ushindi wa mabao mengi bila kuruhusu bao.
“Nafurahishwa na kile wachezaji wangu wanafanya uwanjani, muhimu kwetu ni kupata pointi tatu katika kila mechi, nitaendelea kufanyia kazi vitu vichache hasa eneo la ulinzi na ushambuliaji,” alisema.
Alisema kwa kawaida wanajiandaa na mechi zote za Ligi Kuu zilizobaki, Namungo ikiwa miongoni mwao, hivyo anatarajia watapata matokeo mazuri.
Kwa upande wa Namungo inayoshina nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo, itashuka dimbani ikiwa imetoka kung’ara katika michuano ya Kombe la Shirikisho, ikiifunga Biashara United mabao 2-1, Uwanja wa Majaliwa, Lindi.
Kocha Mkuu wa Namungo, Hitimana Thierry, alisema amewandaa vizuri vijana wake kukabiliana na Simba ingawa alikiri ugumu wa wapinzani wake hao.