Theresia Gasper-Dar es Salaam
UONGOZI wa Klabu ya Yanga, umekamilisha maandalizi ya kikosi chao kwa ajili ya kuvuna pointi tatu dhidi ya Tanzania Prisons.
Timu hizo zitashuka dimbani kesho kuumana, katika mchezo wa Kombe la Shirikisho (ASFC)utakaochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Yanga ilifuzu hatua hiyo, baada ya kuifunga Iringa United mabao 4-0 Uwanja wa Uhuru, wakati Prisons iliiondosha Mlale FC baada ya kuinyuka mabao 4-0, Uwanja wa Sokoine Mbeya.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassan Bumbuli, alisema hali ya kikosi cha timu yake iko shwari na kuongeza kuwa ushindi wao wa mabao 3-1 katika mchezo wao uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida United umepandisha morali ya wachezaji wao.
“Tupo kambini na leo (jana) jioni tutaendelea na mazoezi ya kujiandaa na mchezo huo, benchi la ufundi limeendelea kukiweka kikosi sawa kwani tunakabiliwa na mchezo mgumu na ukifungwa umetoka,” alisema.
Kuhusu majeruhi Tariq Seif alisema, mshambuliaji huyo anaendelea na mazoezi ya peke yake, wakati beki Kelvin Yondan ambaye hakucheza mchezo dhidi ya Singida kutokana na kuugua kifua, ataangaliwa maendeleo ya afya yale leo kabla ya benchi lao la ufundi kuamua kumtumia au la.