FARAJA MASINDE
WATANZANIA wametakiwa kuchangamkia fursa katika vyuo vya elimu ya juu nje ya nchi ili kupata ujuzi unaoendana na mabadiliko ya haraka ya teknolojia.
Wito huo umetolewa jana Dar es Salaam na Mwambata wa Mwenza wa Taasisi ya Elimu ya Juu ya Edugate ya Uingereza, Aliyuthuman Sadhique, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa program maalumu ya kusaidia wanafunzi katika nchi zenye uchumi wa kati inayofahamika kama LICAP.
Alisema program hiyo inalenga kuwafikia wanafunzi na wahitimu mbalimbali kutimiza malengo katika vyuo maalumu vilivyopo Uingereza na Sri Lanka.
“Edugate kwa kushirikiana na Taasisi ya British Colledge of Upplies Studies ya Sri Lanka tumedhamilia kuwekeza katika elimu hapa nchini hususan kuwawezesha watanzania kwenda kusoma nje ya nchi ikiwemo kuwasaidia kimasomo,”alisema.
Aidha, leo Januri 25, katika Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro, itazinduliwa program hiyo ambapo uzinduzi utaaendana na kongamano maalumu litakalo toa fursa kwa watanzania kuzitambua fursa hizo za elimu.
Sadhique alisema kongamano hilo halitakuwa na malipo yoyote na mtu yoyote anaweza kuhudhuria hususan wenye nia ya dhati ya kwenda kujiendeleza nje ya nchi.
Aliwataka wale wote wenye nia ya kusoma nje ya nchi kuhudhuria kongamano hilo na kwamba litakuwa na faida kubwa hususan kwa wahitimu wa Teknolojia ya habari na Mawasiliano (IT), Usimamizi wa fedha, uhandisi na taaluma zingine .
Alisema kwa wale ambao ufaulu wao utaonekana kuwa ni wajuu watasaidiwa kupata udhamini kupitia program hiyo ya LICAP.
Mmoja wa waratibu wa kongamano hilo David Munanka, alisema, mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka ambapo serikali ya awamu ya tano inatekeleza dira yake ya kuelekea uchumi wa viwanda.
“Yeyote mwenye sifa na nia ya kusoma shahada au astahashada nje ya nchi anaweza kuhudhuria kongamano hili bure,”alisema Munanka.