25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Kashfa kubwa zilizong’oa mawaziri

Elizabeth Hombo – Dar es Salaam

KASHFA iliyomng’oa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ni ya pili kwa ukubwa wa kiwango cha ubadhirifu wa fedha tangu Rais Dk. John Magufuli alipoingia madarakani mwaka 2015 na kuunda baraza lake la Mawaziri  na kuwaondoa 17 kwa makosa mbalimbali, MTANZANIA Jumamosi limebaini.

Utafiti uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, hadi sasa kashfa inayoongoza ni ile ya makinikia ambayo ilisababisha kuondolewa madarakani aliyekuwa Waziri wa iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini ambayo sasa imegawanywa, Profesa, Sospeter Muhongo.

Profesa Muhongo aling’olewa na Rais Magufuli Mei 24 mwaka 2017, kwa kushindwa kusimamia vizuri suala la usafirishaji mchanga wa madini (makinikia) kwenda nje ya nchi, hii ikiwa ni mara ya pili mbunge huyo wa Musoma Vijijini kuwajibika baada ya kung’olewa mwaka 2014 katika sakata la Escrow.

Kuhusu kashfa ya makinikia, Profesa Muhongo aling’olewa baada ya ripoti ya tume iliyoongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma kuchunguza kiwango cha dhahabu kwenye makontena yaliyokuwa yamezuiliwa bandarini.

Katika ripoti hiyo, tume hiyo ilisema kampuni ya Acacia iliyokuwa inamiliki migodi mitatu nchini ilitangaza kiwango cha chini cha madini yote yaliyo katika makontena 277 ambayo yalizuiwa kusafirishwa nje kwa amri ya Rais Magufuli.

Matokeo ya tume hiyo yalionyesha thamani ya madini yote yaliyomo ni kati ya Sh bilioni 829.4 na Sh trilioni 1.439 tofauti na thamani iliyotolewa na Acacia ya Sh bilioni 97.5.

KASHFA YA LUGOLA

Kashfa ya pili kwa ukubwa wa kiwango cha ubadhirifu wa fedha, ni ile iliyomg’oa juzi Lugola baada ya viongozi wa wizara yake kutia saini makubaliano ya zabuni ya kununua vifaa vya zimamoto na uokoaji vyenye thamani ya Euro milioni 408.5 (sawa na zaidi ya Sh trilioni 1) kutoka kampuni moja ya nje bila kufuata sheria.

“Kulikuwa na mkataba wa ovyo unaotengenezwa Wizara ya Mambo ya Ndani wenye thamani ya Euro milioni 408, umetayarishwa na kusainiwa na Kamishna Jenerali wa Zimamoto, haujapangwa kwenye bajeti, haujapitishwa na Bunge.

“Wakati wa vikao na kampuni moja ya Romania, wahusika wa Tanzania walipokuwa wanakwenda kwenye majadiliano wanalipwa  ‘seating allowance’ (posho ya vikao) ya Dola 800 na hata tiketi za ndege walilipiwa.

“Yanayokwenda kununuliwa kule kwenye mkataba ni ya ovyo, ni ya ajabu, ukitaka kuuvunja, yale ambayo yameshaanza kutekelezwa lazima yaendelee kutekelezwa,”alisema Rais Magufuli.

Katika kashfa hiyo, Rais Magufuli alimng’oa pia aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto, Thobias Andingenye huku aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu akiandika barua mapema ya kujiuzulu.

Kashfa nyingine inayofuatia kwa ukubwa wa kiwango kikubwa cha fedha ni ile iliyomng’oa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba mwaka 2018 na baadaye nafasi yake kuchukuliwa na Lugola.

Katika kashfa hiyo, Mwigulu alishindwa kushughulikia azimio la Bunge kuhusu suala la kufunga mashine za kielektroniki za utambuzi wa alama za vidole (Afis) katika vituo 108 vya polisi, mradi uliofanywa na Kampuni ya Lugumi kwa gharama ya Sh bilioni 37.

Nyingine ni ile ripoti ya uchunguzi wa biashara ya almasi na Tanzanite iliyomfanya aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene na aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani kujiuzulu.

Simbachawene ambaye sasa ameteuliwa kushika nafasi  ya Lugola aliandika barua ya kujiuzulu baada ya kutajwa katika ripoti ya uchunguzi wa biashara ya madini ya Tanzanite na almasi, iliyoonyesha namna Serikali ilivyopoteza matrilioni ya fedha kutokana na sababu mbalimbali.

Hatua hiyo ilikuja muda mfupi baada ya Rais Magufuli kuwataka viongozi wote ambao wametajwa katika ripoti hiyo wakae pembeni kupisha uchunguzi ambao utakuwa huru na wa haki.

Simbachawene alitajwa katika ripoti hiyo kutokana na kuridhia mabadiliko katika mauzo ya kampuni ya uchimbaji ya Tanzanite na utoaji leseni kinyume na taratibu wakati akiwa Waziri wa Nishati na Madini, nafasi aliyoishika kwa muda mfupi mwaka 2015.

Ngonyani pia alihusishwa na sakata hilo kutokana na kuongoza kamati maalumu iliyoshauri Serikali isinunue hisa za kampuni inayoendesha mgodi wa almasi wa Williamson Diamonds Limited kwa Dola za Kimarekani milioni 10 na kuikosesha Serikali mapato ya Dola za Kimarekani milioni 300 ambazo zimeenda kwa kampuni ya Petra Diamond iliyonunua.

Mawaziri wengine waliondolewa kwa makosa mengine tofauti, ni pamoja na Charles Kitwanga (aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi), ambaye uteuzi wake ulitenguliwa baada ya kuingia bungeni akiwa amelewa.

Nape Nnauye (Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo) naye alitumbuliwa Mei 23 mwaka 2017, siku moja baada ya kupokea ripoti kutoka kwa kamati aliyokuwa ameiunda kuchunguza sakata la kuvamiwa kwa ofisi za Clouds Media Group.

Januari 19 mwaka 2018, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu aliyekuwa akishughulikia walemavu, Dk. Abdallah Possi na kumteua kuwa balozi.

Pia Oktoba 7 mwaka 2018, wakati alipofanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kwa kuongeza idadi ya wizara, alitengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe huku nafasi yake ikichukuliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangala.

Katika mabadiliko hayo, Mhandisi Ramol Makani naye aliachwa na nafasi yake ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii ilichukuliwa na Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga ambaye baadae alipelekwa kuwa Waziri wa Kilimo.

Mwingine ni Anastazia Wambura aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Juliana Shonza.

Septemba mwaka 2018, Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Dk. Susan Kolimba aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kumteua Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Damas Ndumbaro kuchukua nafasi hiyo.

Wengine ni Charles Mwijage (Wizara ya Viwanda) na Dk.  Charles Tizeba (Wizara ya Kilimo) ambao waliondolewa Novemba 2018, kwa kushindwa kushughulikia bei ya korosho, kahawa, pareto na ufufuaji wa Kiwanda cha Chai Mponde kilichopo mkoani Tanga na kile cha Buko mkoani Lindi.

Rais Magufuli alieleza hadharani kuwa hakuona taarifa yoyote ya Waziri wa Viwanda au Kilimo kukemea sekta binafsi.

Alisema kiwanda cha chai kilikaa bila kufanya kazi kwa miaka minane hadi alipomtuma Waziri Mkuu kwenda kutatua tatizo na kwamba Kiwanda cha Mponde na cha Lindi havikurudishwa na wizara na hata mchakato wake mawaziri husika hawakuujua.

Mwingine aliyeondolewa ni Gerson Lwenge aliyekuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji.  

Pia aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda, naye aliondolewa kisha nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa.

Kakunda aliondolewa kufuatia malalamiko yaliyoelekezwa katika wizara yake na wafanyabiashara waliokutana na Rais Ikulu, Dar es Salaam mwaka jana.

Aidha Julai 21 mwaka jana, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba na kumrejesha tena Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene kuchukua nafasi hiyo.

Wakati akimwapisha Simbachawene, Rais Magufuli alitaja sababu za kumng’oa Makamba kuwa ni pamoja na kutotekelezwa kwa wakati kwa katazo la mifuko ya plastiki na kutotumika vizuri kwa fedha zinazotolewa na wafadhili kwa miradi ya mazingira.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,522FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles