Na MWANDISHI WETU
“UNGUJA iliipindua Serikali ya Sultani kibaraka, kwa marungu mama, kwa mapanga mama, mwisho wake wakafaulu.”
Kwenye miaka ya 1960 na 1970 ilikuwa ni rahisi kusikia nyimbo za kumbukizi la Mapinduzi ya Zanzibar ambayo Januari 12, yalitimiza miaka 56.
Mapinduzi hayo ambayo yalijumuisha mambo mengi baadhi yakiwa kwenye kumbukumbu rasmi za kihistoria lakini baadhi yamekuwa yanawekwa pembezoni na hivyo uelewa juu yake kuwa wa juu juu.
Miongoni mwa mambo hayo ni kukosekana kutajwa au kukumbukwa kwa mshiriki mmojawapo kwenye Mapinduzi hayo hali inayoonesha kugubikwa na mwangwi wa kibaguzi ndani ya kumbukumbu za tukio hilo muhimu ambalo limekuwa linaelezwa kuwa ndio chimbuko la kuondoa utumwa na utwana.
Ambaye anaonekana kuwekwa pembeni ni Field Marshal John Okello ambaye kwenye kumbukumbu za kihistoria inaelezwa kuwa aliingia Zanzibar mwaka 1963 na kuwa na mawasiliano na viongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Afro-Shirazi (ASP).
Vijana hao wa ASP inaelezwa kuwa wakiwa wanapanga mbinu za kuuondoa utawala wa Waarabu, Okello kwa upande wake akiwa mwanachama wa chama cha wapiga rangi – akiwa anapaka rangi majumba mbalimbali, katika muda wake wa ziada aliunda kikundi kidogo cha askari wa Kiafrika.
Kikundi hiki cha kijeshi kilishika na kufuata amri alizozitoa Okello kama kiongozi ambazo ni pamoja na kutojihusisha na masuala ya ngono, kutokula nyama mbichi na kutokunywa pombe.
Inaelezwa kuwa Okello alikuwa muumini mzuri wa dini na aliamini kuwa alipewa amri hizo na Mungu akiwa kwenye ndoto ili aweze kuuondoa utawala wa mabavu wa Waarabu na kuanzisha Serikali ya Mapinduzi ya Unguja na Pemba.
Hali kadhalika, inaelezwa kuwa usiku mmoja kabla ya Mapinduzi hayo, Okello aliwaamuru watu wake kuua vijana wote wa Kiarabu waliokuwa na umri kati ya miaka 18 na 25, lakini wasiwadhuru wajawazito na wazee, pia wasifanye ubakaji.
Januari 12, 1964 inaelezwa Okello na kikosi chake waliingia Mji Mkongwe, Zanzibar, maskani ya Sultani, lakini Sultani mwenyewe alikuwa ameshakimbilia mafichoni nchini Uingereza.
Hata hivyo, baada ya kufanikiwa kwa Mapinduzi hayo, Okello alitangaza Baraza la Mapinduzi na Sheikh Abeid Amani Karume kuwa Rais. Kiongozi wa Chama cha Umma, Abdulrahman Mohamed Babu, akawa Waziri Mkuu. Baadaye alikuwa Makamu wa Rais.
Sheikh Karume na Babu hawakuwa wamejulishwa kuhusu Mapinduzi hayo ya kijeshi kwani wote walikuwa Tanganyika, lakini walirudi Zanzibar walikokaribishwa na Okello.
Lakini pamoja na shughuli yote aliyoifanya si Karume wala Babu waliomhitaji tena. Okello aliondoka kuelekea Tanganyika na kuanzia wakati huo alizuiwa kurudi Zanzibar na alipigwa marufuku pia asionekane Tanganyika na Kenya.
Hatimaye inaelezwa kuwa alirudi kwao mara ya mwisho alionekana akiwa na kiongozi wa Uganda Idd Amin Dada mwaka 1971 na baadaye alipotea.
Katika kitabu cha ‘Revolution on Zanzibar’ kilichoandikwa na Don Petterson inadhaniwa kuwa Idd Amin alimwona Okello kuwa ni tishio kwake na mara nyingine inaelezwa kuwa baada ya Amin kujipandisha cheo na kuwa Filed Marshal, inaelezwa kuwa Okello alisema kwa dhihaka, “Uganda hivi sasa ina Field Marshal wawili.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa Idd Amini alipanga mipango ya mauaji dhidi ya Okello, lakini pamoja na hali hiyo kifo chake kimebakia kuwa ni cha utata.
Wapo waliofanya mambo yanayofanana na Okello. Mfano Ernesto Guevara de la Serna maarufu kama Che Guevara, aliyeshiriki kikamilifu kwenye Mapinduzi ya Cuba akiwa ni raia wa Argentina.
Wapo wanaomuona Okello kuwa ni kama askari wa kukodiwa na siku zote askari wa aina hiyo wakimaliza kazi waliyolipwa kufanya huondoshwa haraka.
Yanaweza kuwapo mawazo mengi kinzani kuhusu Mapinduzi, lakini yalikuwa muhimu ili kuleta uwiano wa maendeleo kwa jamii ya Zanzibar ndio maana siku zote kauli mbiu mama imekuwa “Mapinduzi Daima.”