25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Sing’ang’anii kuwa meya, ninachotaka wafuate taratibu – Isaya Mwita

NORA DAMIAN-DAE ES SALAAM

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilimaliza mwaka 2019 kwa furaha kutokana na kufanikiwa kufanya mkutano mkuu uliopanga safu mpya za viongozi wa juu watakaokiongoza kwa miaka mitano.

Safu hiyo pamoja na mambo mengine, ndiyo inayotazamwa kwa karibu na wafuasi wa chama hicho wakati huu wa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba iwapo kitakidhi matarajio ya wanachama au la.

Hata hivyo, zikiwa zimepita wiki mbili tangu kuanza kwa mwaka 2020, upepo wa kisiasa kwa chama hicho umegeuka kutokana na sakata la umeya wa Jiji la Dar es Salaam ambalo limeendelea kuibua mjadala mkubwa.

Mgogoro huo wa umeya umezidi kufukuta baada ya kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kilichofanyika wiki iliyopita katika ukumbi wa Karimjee kumng’oa Isaya Mwita kwa madai ya tuhuma mbalimbali.

Kikao hicho ambacho kilikuwa ni maalumu kwa ajenda ya kumjadili Mwita kiliitishwa baada ya kukamilika kwa ripoti ya uchunguzi dhidi ya Mwita ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Vijibweni.

Katika kikao hicho Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana, aliwasilisha ripoti hiyo na kusoma tuhuma nne zinazomkabili Mwita kuwa ni pamoja na kutumia madaraka yake vibaya kwa kuwaingiza kwenye kamati mameya wa manispaa za Ilala, Temeke, Kinondoni na Ubungo kinyume cha sheria.

Tuhuma nyingine ni kutumia gari kwa matumizi yasiyo ya kiofisi, kushindwa kutekeleza majukumu kwa kushindwa kuzuia fujo na kauli zenye kashfa katika mikutano na kukwamisha matumizi ya Sh bilioni 5.8 zilizotokana na uuzaji wa hisa zilizokuwa za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).

Anasema timu ya uchunguzi ilianza kazi Desemba 13 mwaka jana, na kuikamilisha Desemba 24 kisha iliwasilishwa kwa Mkuu wa Mkoa na ofisi yake ilipokea Desemba 31.

Wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam wakiwa kwenye kikao maalumu kilichokuwa na ajenda ya kumjadili meya

“Matokeo ya uchunguzi ni ishara tosha ya kutozingatiwa kwa taratibu na kanuni za uendeshaji wa vikao. Tume ina maoni yafuatayo…wahusika wachukuliwe hatua stahiki kwa mujibu wa taratibu zilizopo,” anasema Liana.

Baada ya taarifa hiyo, lilifuata zoezi la kupiga kura kisha Naibu Meya wa Jiji, Abdallah Mtinika, alitangaza matokeo kuwa uamuzi wa madiwani umepitishwa na kukifunga kikao hicho.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya wajumbe akiwamo Mwita walionyesha kutoridhishwa na jinsi mchakato huo ulivyoendeshwa na tangu kikao kilipoanza kilitawaliwa na vurugu hali iliyosababisha kifanyike chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Mzozo mkubwa ulikuwa katika suala la akidi kwamba haijatimia kama zinavyoelekeza kanuni ambazo zinataka kuwe na theluti mbili iwapo wajumbe wanataka kumng’oa meya.

Mara kwa mara Mwita alikuwa akimuomba mwanasheria kutoa mwongozo kuhusu suala la akidi na mambo mengine ili kutenda haki kwa kila upande. 

WAJUMBE WALIOKUWAPO

Baraza hilo lina wajumbe 26 yaani wabunge watano, mameya sita na wajumbe wengine 15 na ili kupata theluthi mbili ni watu 17.

“Kupata theluthi mbili ni watu 17, kilichofanyika hapa Mshamu (Diwani wa Kata ya Minazi Mirefu) hayupo, haiwezekani huu ni uhuni, mtu amesainiwa ionekane akidi imetimia,” anasema Mwita.

Aidha baadhi ya wajumbe walidai kuwa kuna hujuma zimefanyika kwa kumuandika mjumbe huyo kutoka Chama cha Wananchi (CUF) wakati yuko nje ya nchi.

Huku akiwa ameshika daftari la mahudhurio, Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob, alisimama pamoja na Diwani wa Kata ya Tabata, Patrick Asenga, na kudai kuwa sahihi ya Mshamu imegushiwa wakati hajahudhuria kikao hicho.

“Kuna mjumbe hayupo lakini amesainiwa, hii ni forgery (kugushi), mkurugenzi toa ufafanuzi mtu hayupo amesaini vipi?…Hiki ni kikao cha Serikali uhuni umefanyika,” anasema Jacob.

Akijibu hoja mbalimbali za wajumbe kuhusu suala la akidi, kuna wakati Mkurugenzi alisema wajumbe waliosaini daftari ni 19 na baadaye tena alisema alihesabu vichwa hakuangalia daftari lakini kwa busara alisema kikao kianze.

Mwanasheria alisema kanuni ya 84 katika tangazo la Serikali namba 417 la 2014 inasema meya anaweza kuondolewa madarakani kwa azimio linaloungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe wa halmashauri.

 “Akidi inahesabiwa kutokana na daftari la mahudhurio. Kanuni ya 12 (ii) inasema akidi katika mkutano maalumu wa halmashauri itakuwa ni theluthi mbili,”anasema mwanasheria huyo.

Kisha kikao kilimuomba mwanasheria awaongoze namna ya kupiga kura ambapo alisema kwa kuwa tuhuma dhidi ya meya huyo zilishajadiliwa wanaweza kupiga kura au kumhoji mtu mmoja mmoja.

Mkurugenzi anasema waliandaa karatasi kwa ajili ya kupiga kura ya wazi lakini wakati akiendelea kuongea Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaurembo, alisimama na kumkatisha.

“Hatuna haja ya kupiga kura, ukisoma tuhuma ya kwanza hadi ya nne zina mashiko. Amesababisha hasara ya zaidi ya Sh milioni 20 kwa kuingiza mameya kwenye kamati.

“Mwenyekiti tumeridhia madiwani tulio wengi hatuna imani na mstahiki meya,” anasema Chaurembo.

Baada ya hoja hiyo wajumbe walipiga kura ya wazi ambapo waliounga mkono meya kung’olewa walisimama.

Kisha Naibu Meya, Mtinika alisimama na kutangaza matokeo ambapo alisema kura zilizopigwa ni 16, mjumbe mmoja ametoa udhuru na wajumbe wawili hawajapiga kura.

“Uamuzi wenu umepitishwa na kikao nimekifunga,” anasema Mtinika.

ALIPATA TAABU WAKATI WA KUINGIA

Mwita anasema wakati anagombea nafasi hiyo alikumbana na mikiki mikiki mingi na hata sasa anataka kutolewa kwa njia hiyo hiyo.

Isaya Mwita (wa pili kutoka kushoto), akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu juzi

“Hadi sasa hawajapata uhalali wa kuniondoa kanuni ziko wazi, kwenye kuingia nilipata hivi hivi sukuma sukuma na sasa natokakwa mtindo huu. 

“Namuomba mheshimiwa John Magufuli tumeapa kulinda kanuni na miongozo aingilie suala hili kwa sababu ni jambo la aibu.

“Nawaomba sana viongozi wa dini waendelee kuniombea katika zoezi hili, mimi siishii hapa, naendelea kupigania haki yangu kwa sababu naamini nawapigania Watanzania wote wa Mkoa wa Dar es Salaam waliopiga kura wakanileta hapa,” anasema Mwita.

Anasema yeye bado ni meya halali kwani taratibu zilizotumika kumuondoa ni batili.

“Theluthi mbili ya baraza ndiyo inapaswa kuniondoa lakini kilichotokea wajumbe waliohusika ni 16, waliounga mkono ni 13 na sisi tuliokataa ni wawili na mmoja alikuwa ametoka nje.

 “Sing’ang’anii kuwa meya lakini nataka wafuate taratibu ndiyo maana walipotaka wapate theluthi mbili walimuomba mheshimiwa Mshamu awasaidie, leo amesafiri anauguza hayupo nchini. Wangempata akawa mtu wa 17 uhalali wa kuniondoa ulikuwepo.

 “Naona bendera imeshashushwa kwa maana kwamba hata gari lenyewe nimeshanyang’anywa, ni aibu sana kama tumefika hapa,” anasema.

MTIRIRIKO WA MATUKIO

Kikao hicho kilitawaliwa na vurugu zilizosababisha kisimame mara kwa mara. 

Mwita akiwa ameambatana na Jacob na Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, waliingia ukumbini ikiwa ni saa chache (saa 4:42 asubuhi) baada ya kuanza kusomwa kwa ripoti ya uchunguzi.

Kisha alikwenda kukaa katika kiti chake na baada ya mkurugenzi kumaliza kusoma taarifa hiyo alisimama naibu meya na kuelekeza uamuzi ufuate.

Kabla kikao hakijaendelea Meya Chaurembo aliomba mwongozo akitaka kujua iwapo meya huyo ataachia kiti au ataendelea wakati akijadiliwa.

“Yeye (Meya) ni mtuhumiwa hatakiwi kuongoza kikao, anaacha wajumbe wa chama chake wafanye fujo. Tupishe mstahiki meya mimi ndiyo katibu, ukae kule,” anasema Sipora.

Hata hivyo Mwita aligoma kutoka kwenye kiti na kusema; “Ikifika ajenda ya kunijadili nitakaa pembeni, nimekwenda shule najua lengo letu tumalize salama.

“Naibu (Mtinika) naomba usinitishe kama nitaondolewa nitakuachia uendeshe kikao.

Kuna wakati pia Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea (CCM), alimtaka Mwita achague mawili ama asaini mahudhurio au aachie kiti akishuhudia shughuli za baraza zikiendelea.

Hata hivyo Mkurugenzi alisema Mwita alipoingia tu alisaini lakini aliomba achelewe kikao kwa dakika 20 ili awasubiri wajumbe wa chama chake.

Tukio lingine ni la Diwani wa Tabata, Asenga ambaye alikamatwa na polisi baada ya kudaiwa kufanya fujo katika kikao hicho. 

AONDOA KESI MAHAKAMANI

Awali Mwita aliwafikisha mahakamani Halmashauri ya Jiji, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mwanasheria Mkuu wa Serikali akipinga kuondolewa katika nafasi yake.

Hata hivyo juzi aliamua kuiondoa kesi hiyo mahakamani kwa kile alichodai kuwa mkakati wa kumuondoa umekwama kama sheria inavyotaka hivyo bado ataendelea kuwa meya. 

Anasema kwa sasa ameamua kurudi kwa wananchi ili waamue hatima yake na kwamba hatorudi nyuma katika kupigania heshima ya wananchi wa Dar es Salaam.

“Kesi nilifungua Januari 8 ili kuzuia jambo lolote la kuniondoa, lakini Januari 9 kikao kimefanyika lakini waliotaka kuchukua uamuzi walikwama kutokana na kukosekana akidi.

“Sasa nimeona ya nini kuendelea na kesi kwani sijaondolewa kwenye umeya hadi sasa kwa mujibu wa sheria. Nitaendelea kuhudumia wananchi wangu wa Jiji la Dar es Salaam pasi na hofu,” anasema Mwita.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyokuwa ikisikiliza maombi hayo ilimwamuru Mwita kulipa gharama za kesi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,430FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles