23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

Mwanamume ni kichwa cha familia, hatakiwi kuzira

Na CHRISTIAN BWAYA

KAMA uliwahi kucheza ile michezo ya utotoni, utakubaliana nami kuwa hakukuwa na maumivu makali kama mwenzenu mnayetegemea mpira wake kuwaziria mchezo.

Ilikuwa inaumiza pale ambapo kuna hali ya kutokuelewana imejitokeza mara mwenzenu anawatishia, “Sichezi na nyie.”

Nyakati kama hizi baadhi yetu tulitamani wazazi wetu wangekuwa na uwezo wa kutununulia mpira mwingine na sisi tuoneshe makeke. 

Si kila mtoto alikuwa na uwezo wa kuzira. Nguvu ya kuzira ilitegemea kile ulichonacho.

Mwenye sarafu zaidi kwa ajili ya kununulia ‘bazoka’, mwenye rangi za kuchorea, mwenye kamba ya kurukia, mwenye ujuzi mfano mtaalam wa kutengeneza magari  au mwenye chochote kile ambacho  kina nyie inabidi muwe wapole kupata huruma yake ndiye alikuwa na uwezo wa kuzira.

Kuzira ilikuwa namna ya kushinikiza madai yake yatekelezwe na nyie wengine ambao bila yeye mchezo unakuwa umeharibika.

Hali ilikuwa mbaya pale ambapo mnakuwa mmetengeneza timu za kushindana na mwenye mpira anaona kabisa safu aliyonayo haina uwezo wa kushinda basi anaamua kutumia rungu lake la ‘sichezi na nyie’ ili tu mlazimike kupangua safu.

Watoto ‘wanyonge’ walikuwa hawana la kufanya lakini wale wabishi, tishio kama hili halikuwa linakubalika.

Ukisema ‘sichezi na nyie,’ wanakwambia, ‘isiwe tabu nenda kwenu.’ Usitake kutukalia kichwani kisa wewe ndiye mwenye mpira wa ‘dukani.’

Kwa vichwa ngumu kama hawa ilikuwa bora kutengeneza mpira wa matambara kuliko kuendeshwa na ‘mhisani’ anayetaka kuharibu mchezo kulinda maslahi yake.

Nimekumbuka enzi hizo baada ya kusikia simulizi za watu wazima kuzirana. Sikuwahi kufikiri mwanamume anaweza kufanya michezo hiyo ya kitoto. Mume anarudi nyumbani hataki kula.

Mume anaamua kuchelewa kurudi nyumbani kwa sababu anataka kumnyoosha mke wake. Mume anakata mawasiliano na mke wake kwa sababu tu kuna vitu hawajakubaliana.

Hivi unaweza kuamini kuna wanaume wanafikia hatua ya ‘kuwa-block’ wake zao kwenye mitandao ya simu?

Unauliza kisa unaambiwa, ‘Nataka kumshikisha adabu yake.’ Unaanzaje kumzira mke wako hata kama amerudia kosa hilo mara kadhaa?  

Ukiangalia tabia kama hizi unakuta mwanamume huyu anayekimbilia kuzira  zira mara nyingi anakuwa na kitu anaficha.

Haitokei hivi hivi. Mtu, mathalani, ameshindwa kumpenda mke wake kama alivyokuwa anampenda enzi za uchumba, mke amebaki mpweke anayeishi kama kuku wa kienyeji.

Hana matumaini ya kupata mapenzi aliyoyaota enzi za usichana wake lakini akilalamika kidogo, mume anamrudisha kule kule kwenye michezo ya kitoto ‘sichezi na wewe.’

Badala ya kutatua tatizo, mume anaamua ‘sasa sirudi nyumbani tuone nani mjanja,’ ‘sitoi hela ya matumizi tuone nani mwanamume humu ndani.’ Unajiuliza, kuchelewa kuja nyumbani, kuacha kumpenda mke wako, kusitisha mawasiliano na mkeo, ndio ufumbuzi wa tatizo? 

Shida moja wapo ya kuzira ni kumfanya anayezirwa afikirie kulipiza kisasi zaidi. Inakuwa mchezo wa kutunishiana misuli kama tulivyofanya enzi za utoto.

Mke anaamini hatendewi haki, mume naye anaamini hatendewi haki. Wote wawili wanaamini wamekosewa na aliyewakosea lazima awajibike.

Mume amezira na mke anajisikia kadharaulika. Mara nyingi kwa sababu mke anakuwa mnyonge kidogo kuliko mume atalazimika kujisumbua kidogo lakini naye baada ya muda anaamua kutafuta ustaarabu wake.

Mume aliyezira anapoona mke naye ‘amezira’ huchukua hatua ya kurudisha lawama.

‘Kwanini hufanyi hiki na kile.’ Hali inapofikia hapa, sote tunajiuliza, nani hasa wa kuchukua hatua kunusuru matatizo? Jamii yetu imetupa mahali pa kuanzia. Familia zetu zina muundo wa uongozi wa familia uliokubalika.

Mume, kwa mfano, anachukuliwa kuwa ndiye kichwa cha familia.

Mke kwa upande wake anatarajia mume wake asiishie tu kujiita kichwa cha familia bali aoneshe kwa vitendo kwamba yeye kweli ndiye kichwa cha familia. 

Kichwa cha familia sio madaraka bali majukumu. Jamii yetu imemkabidhi mwanamume majukumu muhimu kama vile kutunza familia yake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha migogoro inayojitokeza inapatiwa ufumbuzi wake kwa wakati.

Katika mazingira ambayo familia inakabiliwa na mgogoro, mwanamume ndiye anayetegemewa kuonesha uongozi kwa kuchukua hatua badala ya ‘kuzira’.

Mwanamume hawezi kukwepa kazi ya kumpenda mke wake. Hawezi kukwepa kazi ya kumsikiliza mke wake.

Hawezi kukwepa kuhakikisha dukuduku linaloisumbua nafsi ya mke wake linasikilizwa.

Hata kama ni kweli mke anaweza kuwa chanzo cha mitafaruku kwenye familia, hatima ya yote anayewajibika kuhakikisha kuwa ufumbuzi unapatikana ni mwanamume.

Kuzira, kususa, kujihami, kukimbia familia, hiyo haiwezi kuwa tabia ya mwanamume anayetarajiwa kuwa kichwa cha familia.

Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya Simu: 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,712FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles