Na MWANDISHI WETU- DODOMA
KATIBU Mkuu Wizara ya Afya – Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. John Jingu, amewataka wadau wa utoaji huduma kwa wazee kutoa maoni ya kuboresha Sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003 ili kukidhi mahitaji ya wazee ambao wamelitumika taifa kwa bidii na maarifa pindi walipokuwa na nguvu na sasa wanapata huduma, fursa na kuenziwa.
Dk. Jingu alisema hayo wakati wa kufungua kikao cha wadau wa kitaifa waliokutana Dodoma kwa lengo la kuhuisha Sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003 ambayo inapitiwa, kujadiliwa na kupokea maoni kuhusu uhalali wa matamko na maelekezo ya kisera kwa kuboreshwa ili kuwapa fursa ya kuendelea kutoa mchango katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa mtaalamu mwelekezi Dk. Richard Sambaiga ameandaa rasimu ya awali ya sera hiyo itakayotumika kuchochea fikra za wadau ili kupata maoni chanya yatakayojumuishwa katika sera iliyoboreshwa itazingatia mazingira halisi ya afya, ulinzi, usalama, hifadhi ya kijamii, matunzo na ushirikishwaji katika masuala ya kijamii.
Katika kutekeleza Sera ya Wazee ya Mwaka 2003, alisema kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhudumia wazee, ikiwa ni pamoja na kusimamia makao ya wazee 17 yanayomilikiwa na Serikali ambayo hivi sasa yamepunguzwa manne na kubaki 13.
Dk. Jingu alisema lengo ni kuboresha huduma kwa wazee wasiojiweza, wanaoishi katika makao hayo baada ya familia zao kushindwa kuwapa huduma za msingi.
“Katika mazingira ya kawaida, Serikali inachukua jukumu la kuwalea wazee baada ya kuthibitika kuwa familia husika haina uwezo au haikujitokeza kutoa huduma,’’ alisema Dk. Jingu.
Aidha alisistiza kuwa wajibu wa kulea wazee wasiojiweza haukomei tu kwa familia, bali ni jukumu linalohusisha pia jamii kwa ujumla, hivyo amewataka wadau wote kutambua kuwa kila mtu ana mchango katika malezi na matunzo ya wazee hapa nchini.
Mpango wa utambuzi wa wazee katika halmashauri hadi kufikia Desemba mwaka jana umewezesha kuwatambua jumla ya wazee 1,837,162 (wanaume 834,595, wanawake 1,002,567). Kati yao wazee wasio na uwezo 684,383 (wanaume 348,171, wanawake 336,212) wamepatiwa vitambulisho vya matibabu bila malipo.
Naye Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Dk. Naftali Ng’ondi alisema ni muhimu kuboresha sera ya wazee ili kuakisi mahitaji na changamoto zinazowakabili wazee kwa mazingira ya sasa maana sera iliyopo ni ya miaka16 iliyopita.