27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Unavyoweza kuepuka saratani ya matiti

AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM

SARATANI ni ugonjwa usio wa kuambukiza ambao unatokana na mtindo mbaya wa maisha hasa ukihusishwa na aina ya ulaji na unywaji.

Ugonjwa huo kwasasa unatajwa kuwa hatari zaidi duniani kwa kusababisha vifo vya watu hii ni baada ya kutokutibika kabisa endapo mgonjwa hatawahi hospitali.

Saratani zipo zaidi ya 200 lakini kuna zile ambazo zinaongoza kuwapata watu hasa wanawake ndio wahanga wakubwa.

Saratani ya mlango wa kizazi inashika nafasi ya kwanza kwa asilimi 56 ambapo Mkoa wa Mbeya unaongoza wakati saratani ya matiti inashika nafasi ya pili kwa asilimia 14 baada ya kupanda kutoka nafasi ya nne.

Saratani ya tatu ni ya njia ya chakula na ya nne ni ya ngozi ikifuatiwa na saratani ya inyounganisha sehemu za kichwa na shingoni, tezi, saratani ya damu, tezi dume, kibofu cha mkojo na ngozi inayowaathiri wenye ualbino.

HALI ILIVYO

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Tafiti za Saratani (IARC) na Shirika la Afya Duniani (WHO) zilizotolewa mwaka jana, zinaonyesha watu zaidi ya milioni 43.8 duniani wanaishi na saratani na kila mwaka kunatokea wagonjwa wapya wanaokadiriwa kufikia milioni 18.1.

Kati ya hao zaidi ya wagonjwa milioni 9.6 hufariki na inakadiriwa kutakuwa na wagonjwa wapya milioni 24 ifikapo mwaka 2035.

Kwa hapa nchini takwimu hizo zinaonyesha kunatokea wagonjwa wapya wa saratani 42,060.

Takwimu za hospitali zinaonyesha wagonjwa wapya 14,028 walihudumiwa mwaka 2018 ambao ni sawa na asilimia 33.3 ya wagonjwa wote nchini.

Wagonjwa waliofika kupata huduma Ocean Road ni 7,649, Hospitali ya Bugando 2,790, KCMC 1050, Muhimbili 1,321 na Mbeya Rufaa ni wagonjwa 218.

Hata hivyo takribani wagonjwa 1000 walipata huduma katika hospitali binafsi za Aghakan, Hindu Mandal, Hubert Kairuki, Besta, Rabininsia na mikoani.

Sababu zilizotajwa na wizara kuongezeka kwa ugonjwa huo ni mabadiliko ya sayansi na teknolojia huku mitindo tofauti ya maisha ikijumuishwa.

SARATANI YA MATITI

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk. Julius Mwaiselage, anasema saratani ya matiti imekuwa changamoto kubwa kutokana na kuongezeka siku hadi siku.

Anasema Mkoa wa Dar es Salaam ndio unaoongoza kwa kuwa na saratani hiyo huku chanzo kikiwa na wanawake kuzaa watoto wachache na kukwepa kunyonyesha.

Anataja sababu zingine hasa kwa maeneo ya mijini kuwa ni mtindo na mfumo mbaya wa maisha, uzito uliopitiliza, kutofanya mazoezi na matumizi ya pombe na sigara.

“Saratani ya matiti inaendelea kuongezeka kwa kasi, tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi tuhanamasisha uonyenyeshaji ili kupunguza vichocheo vinavyoenda kuathiri matiti.

“Kingine ni kuwa na watoto wa kutosha, huku mjini mtu anakuwa na mtoto mmoja au wawili lakini ukiwa na watoto kuanzia wanne uwezekano wa kupata saratani ya matiti unapungua. Tunaendelea kuhamasisha upimaji kwa wanawake na watoto,”anasema Dk. Mwaisalage.

UFANYE NINI?

Akielezea namna uzazi unavyosaidia kuepukana na saratani ya matiti, Daktari Bingwa wa Saratani, Crispin Kahesa, anasema mwanamke anapozaa homoni za uzazi za estregen zinakuwa katika uwiano unaolingana ambapo hali hii huepusha saratani.

“Mwanamke kuzaa kunaendana na mzunguko wake wa hedhi hivyo vyote vinasababishwa na homoni, mama anapozaa homoni zina – ‘balance’ na mama ambaye hazai kuna baadhi ya homoni hazi – balance hasa zinazohusishwa na saratani ya matiti za estrogen.

“Hizi lazima ziwe na uwiano mzuri, kuzaa kunasaidia homoni ziweze ku – balance vichocheo vya mwili vizuri.

“Vichocheo hivyo havitakiwi kukatizwa, vikikatizwa vinaleta mabadiliko yasiyo sahihi kwenye chembechembe za matiti kwa hiyo vinaweza  kuongeza hatari ya saratani ya matiti,”anasema Dk. Kahesa.

Anasema ni vema wazazi wakaongeza idadi ya watoto ili wanawake waweze kujitoa katika vihatarishi vya kupata saratani hiyo.

VYAKULA VILIVYOKAUSHWA

Ulaji wa vyakula vinavyokaushwa huweza kusababisha saratani ya ini kutokana na vyakula hivyo kuwa na uwezo wa kuzalisha sumu kuvu.

“Kuna saratani inatokana na uhifadhi wa chakula au kinavyokaushwa iwe mahindi, mihogo, uwele ambao haujahifadhiwa vizuri hivi vinaweza kutengeneza sumu kuvu na kusababisha saratani ya ini na hizi zinatokea sana ukanda wa kati,” anasema.

MAFANIKIO UTOAJI TIBA

Dk. Mwaisalage anasema ununuzi wa vifaa tiba na mashine za tiba ya mionzi zilizogharimu Sh bilioni 9.5 umesaidia kurahisisha matibabu ya saratani ndani ya nchi.

“Kwasasa tumekuwa na huduma bora tofauti na zamani, wagonjwa wanaendelea kuongezeka hii inatokana na baada ya kupata elimu na hasa ya kwenda hospitali kupima na kupata matibabu.

“Tumepata mashine mbili za mionzi za kutibu saratani na tangu zimefungwa Septemba mwaka jana tumeweza kuhudumia wagonjwa 1,141.

“Tiba ya mionzi imesaidia sana mwaka 2015 tulikuwa tunawapatia matibabu wagonjwa 30 tu lakini sasa wagonjwa wanafikia 70 kwa wiki,” anasema.

Anasema kuwa uwepo wa mashine hizo kumeokoa Sh bilioni 10.4 kutokana na wagonjwa hao kutibiwa ndani ya nchi.

Mkurugenzi huyo anasema pia kulifanyika ujenzi wa jengo ambao uligharimu Sh bilioni 2.3 na uboreshaji wa miundombinu mingine ya taasisi na kwamba ujenzi huo umeongeza wodi za wagonjwa na mpaka sasa vitanda vya kulala vimefikia 270.

 Dk. Mwaisalage pia anasema huduma za dawa zimeimarika ambapo bajeti ya ununuzi wa dawa imeongezeka kutoka Sh milioni 77 hadi Sh biloni 10.

“Kulikuwa na upungufu wa dawa lakini sasa dawa zipo, mwaka 2015 dawa za saratani zilipatikana kwa asilimia nne lakini kwa sasa upatikanaji wake ni asilimia 95 hili ni ongezeko kubwa zaidi,”anasema.

Mkurugenzi huyo anasema tayari Serikali imetoa Sh bilioni 14.5 kwa ajili ya ujenzi wa jengo, ununuzi na usimikaji wa kiwanda cha Cyclotron kwa ajili ya kuzalisha dawa za nyuklia.

“Upatikanaji wa vipimo hivi nchini utapunguza gharama za kupeleka wagonjwa nje ya nchi hivyo Serikali itaokoa Sh bilioni 5 kwa mwaka,” anasema.

Anasema mradi huo utakamilika mwakani na tayari wataalamu wenye uwezo wa kuzitumia wameshaandaliwa.

“Hii itakuwa mashine kubwa kwa Ukanda wa Afrika Mashariki hivyo tutapata wagonjwa hata wa nje ya nchi,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles