25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Makonda aanika Dar mpya, viongozi wa dini wanena

Waandishi Wetu – Dar es Salaam

MKOA wa Dar es Salaam umevunja rekodi ya kujenga mtandao wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 807 ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli. 

Akizungumza na viongozi wa dini jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika, hadi Desemba 2015 barabara zilizojengwa zilikuwa kilomita 402 tu.

Alisema tangu kuingia Serikali ya awamu ya tano, imejenga barabara mara mbili na kuzifanya kufikia 1,209.

Alisema kiwango cha changarawe zimejengwa kutoka kilomita 985.87 hadi kilomita. 1,170.68 sawa na ongezeko la kilomita 181.31; kiwango cha udongo kutoka kilomita 2,798.13 hadi kilomita 2,979.44 sawa na ongezeko la kilomita 181.31.

“Maboresho katika makutano ya Barabara ya Morogoro na Mandela (Ubungo), ujenzi wa ‘Interchange’ ya Ubungo umefikia asilimia 55. Kwa sasa ujenzi wa madaraja ya kuelekea barabara za Sam Nujoma na Mandela unaendelea.

 “Gharama ya mradi ni Sh bilioni 200.7 na utakamilika Julai 22, mwakani,” alisema Makonda. 

Alisema mradi wa upanuzi wa Barabara ya Bagamoyo sehemu ya Morocco hadi Mwenge yenye urefu wa kilomita 4.3 utakamilika Februari, 2021 kwa gharama ya Sh bilioni 69.759 na hadi sasa  maendeleo ya mradi ni asilimia 21. 

“Ujenzi wa awamu ya pili ya miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT System) katika barabara za Kilwa, Bandari, Gerezani, Sokoine, Chang’ombe na Kawawa umeanza Machi mosi, mwaka huu na utakamilika Mei 5, 2022 kwa gharama ya Sh bilioni 234.250 ambapo mpaka sasa umefikia asilimia 10,” alisema Makonda.

Alisema upanuzi wa njia nane wa Barabara ya Morogoro (Kimara – Kibaha), ujenzi umefikia asilimia 50 kwa gharama ya Sh bilioni 140.449, na utakamilika Januari 20, 2021.

“Ujenzi wa daraja jipya la Salender umefikia asilimia 17. Gharama ya mradi ni Sh 243,750,344,664.00 na utakamilika Oktoba 14, 2021.

“Ujenzi wa Barabara ya Tegeta Kibaoni – Wazo Hill – Goba kwa kiwango cha lami (sehemu ya Goba hadi Madale kilomita 5.0), umekamilika kwa gharama ya Sh bilioni 10.241 ambapo ujenzi wa sehemu ya pili ya barabara hii kuanzia Madale mpaka Wazo (kilomita 6), umeanza Novemba mosi, mwaka huu na utakamilika baada ya miezi 18 kwa gharama ya Sh bilioni 9.946,” alisema Makonda.

Aliongeza ujenzi wa barabara ya Samaki Wabichi (Tangi Bovu) hadi Goba yenye urefu wa kilomita 9 umekamilika kwa gharama ya Sh bilioni 8.679.

“Ujenzi wa barabara kuanzia Goba mpaka Mbezi Luis (Mbezi Mwisho) yenye urefu wa kilometa 7 umekamilika kwa gharama ya Sh bilioni 6.768, huku ujenzi wa barabara ya Kinyerezi – Kifuru – Malambamawili – Msigani  – Mbezi Luis (Mbezi Mwisho) yenye urefu wa kilometa 12 umekamilika kwa gharama ya Sh bilioni 25.564,” alisema.

Makonda alisema ujenzi wa barabara ya Tabata Dampo yenye urefu wa kilomita  1.6 umekamilika kwa gharama ya Sh bilioni 1.806 huku ujenzi wa barabara ya Msewe hadi Chuo Kikuu yenye urefu wa kilometa 2.6 umekamilika kwa gharama ya Sh bilioni 2.633 na ujenzi wa Daraja la Mlalakuwa pamoja na barabara za maungio umekamilika kwa gharama ya Sh bilioni 4.949. 

“Ujenzi wa barabara ya Banana – Kitunda – Kivule – Msongola sehemu ya Kitunda – Kivule (km 3.2), umeanza Oktoba mosi, mwaka huu na utakamilika baada ya miezi kumi na mbili kwa gharama ya Sh bilioni 5.900 ambapo mpaka sasa umefikia asilimia 5,” alisema Makonda.

Alisema awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara ya Ardhi – Makongo – Goba kwa kiwango cha lami kuanzia Goba hadi Makongo Juu umekamilika kwa gharama ya Sh bilioni 7.736, na awamu ya pili ya ujenzi wa barabara hiyo imeanza Novemba mosi, mwaka huu na utakamilika baada ya miezi kumi na mbili kwa gharama ya Sh bilioni 8.149.

Makonda alisema miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Kibada – Mwasonga – Tundwisongani – Kimbiji yenye urefu wa kilometa 41 na barabara ya Mjimwema – Kimbiji – Pemba Mnazi yenye urefu wa kilomita 30 imeanza kutekelezwa.

Akizungumzia miradi iliyotekelezwa alisema Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP) unatarajiwa kujenga kilometa 189.669 kwa kiwango cha lami.

“Halmashauri ya Manispaa Temeke zitajengwa kilometa 80.177, Halmashauri ya Manispaa Kinondoni kilometa 51.831 na Halmashauri ya Manispaa Ilala kilometa 57.661.

“Mradi huu utakapokamilika utagharimu kiasi cha Sh bilioni 457.3,” alisema Makonda.

Alisema utekelezaji wa mradi huu uko katika hatua mbalimbali ambao utajumuisha ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami, ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua, maboresho ya mito, ujenzi wa masoko na viwanja vya mpira.

“Mpaka sasa ujenzi wa miundombinu ya barabara yenye urefu wa jumla ya kilomita 143 na ujenzi wa ofisi tatu, maabara tatu pamoja na vifaa vya maabara umeshakamilika,” alisema Makonda.

Alisema utekelezaji wa miradi ya DMDP unategemea kukamilika mwaka 2020 na hivi sasa upo hatua mbalimbali,” alisema Makonda.

Kuhusu afya, Makonda alisema vituo saba vya afya vyenye uwezo wa kufanya upasuaji, hospitali nne zimejengwa, mbili zimekamilika na mbili ujenzi wake umeanza, ambazo ni Hospitali ya Wilaya ya Ubungo na Kinondoni.

Alisema kwa sasa kumekuwapo ongezeko la umeme wa uhakika kutokana na kukamilika kwa miradi mikubwa ya umeme ambayo ni Kinyerezi awamu ya kwanza A na B.

“Kwa sasa wafanyabiashara wa Mkoa wa Dar es Salaam hawatakuwa na mashaka juu ya kukatika kwa umeme mara kwa mara,” alisema.

VIONGOZI WA DINI

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Alhad Salum amewataka viongozi wote kuondoka na tamko la kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli pamoja na Makonda.

Alisema wapo watu ambao hawaoni haya na kupinga juhudi hizi kutokana na upofu walionao, wanatakiwa kuwaombea wapone waweze kuona.

“Kuna wakati demokrasia inatupa shida kipindi ambacho tunahitaji zaidi maendeleo yaendelee,” alisema Sheikh Alhad.  

Askofu Dayosisi ya Mashariki na Pwani wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa alisema katika kufanya jambo lolote lile lazima upitie mishale kama utasimamia katika haki.

“Sisi tungebaki wananchi na viongozi wa dini wa Mkoa wa Dar es Salaam, tusingefanya hivi, kitu ulichokifanya kinatuzidishia ukaribu na kinaonyesha dhahiri tunahusika kwa kila hatua kwa haya tunayoyaona, tunakushukuru, hatutakuwa wakweli kama hatutalisimamia jambo hili na kuwa wakweli kwako.

“Tunajua katika kusimamia jambo lolote kunakuwa na mishale, hasa katika kusimamia haki na ukweli, yawezekana pia wewe ukaona mishale inakuja kwako, lakini kwa kuwa upo nasi viongozi wa dini tutakuombea, tunajua mchango wa shughuli nzuri unazozifanya katika mkoa wetu, tunahitaji kuweka mkakati katika miradi unayoifanya,” alisema Askofu Malasusa.

Alisema mishale mingine alipigwa wakati wa suala la dawa za kulevya, lakini viongozi wa dini walikuwa upande wake hadi kumalizika kwa janga hilo. 

Naye Askofu mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alisema hivi karibuni katika mitandao ya kijamii kumezuka maneno kuwa  Rais Dk. Magufuli ni dikteta.

“Na sababu ya kuitwa hivyo ni yale anayoyafanya, anashughulikia zaidi kuendeleza vitu kuliko kuendeleza watu, wapo watu wananiambia yanayoandikwa kwenye mitandao kama kuna swali la dikteta ningependa wataalamu watuelezee nini maana ya neno hilo.

“Tunahitaji kuwa na viongozi wengi kama Magufuli na Makonda ili hata akiondoka wawepo wengi waadilifu watakaoweza kuziba pengo lake,” alisema Pengo.

Habari hii imeandaliwa na TUNU NASSOR, BRIGHITER MASAKI na FERDINANDA MBAMILA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles