20.8 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Majaliwa amtaka mtendaji mkuu TBA ajitathmini

Mwandishi Wetu -Dodoma

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Daud Kondoro ajitathmini kuhusu utendaji kazi wake, huku akiwasimamisha kazi wakurugenzi watatu wa wakala huo.

“TBA tunaihitaji, watu wake wana shida. Hatuwezi kuwaacha, wasipewe miradi kwa sababu hawawajibiki na wanadhani kwa kuwa ni taasisi ya Serikali ndio wataachwa wafanye mambo ya ovyo,” alisema.

 Majaliwa aliwasimamisha kazi wakurugenzi hao jana alipotembelea mradi wa ujenzi wa ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) eneo la Njedengwa, Dodoma.

Wakurugenzi waliosimamishwa kazi ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ujenzi, Humphrey Killo, Kaimu Meneja wa Miradi, Abdallah Awadh na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushauri, Hamis Kileo.

Majaliwa alichukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na utendaji kazi wa wakala huo katika miradi mbalimbali waliyopewa na Serikali, ukiwamo ujenzi wa jengo la NEC ambao ulianza Julai, 2017 na ulitakiwa ukamilike Juni, 2018 kwa gharama ya Sh bilioni 13. Hata hivyo mradi huo bado haujakamilika na ujenzi wake umesimama.

Akiwa eneo la mradi wa ujenzi, Majaliwa alihoji sababu za kutokamilika kwa wakati na kaimu mkurugenzi wa ujenzi alisema jengo hilo limeshindwa kukamilika kwa sababu wakati walipokuwa wanaanza kazi walibaini kuna vitu vilisahaulika wakati wa uandaaji wa Bill of Quantities (BOQ). TBA ndio waandaaji wa ramani ya jengo hilo na ndio wajenzi.

“Bajeti ya awali ilikuwa Sh bilioni 10, wakati wa uandaaji wa michoro ya ujenzi gharama ziliongezeka na kufikia Sh bilioni 13 ambazo ndizo tulikubaliana katika mkataba.

“Wakati tunaendelea na kazi tuligundua kuna vitu vimesahaulika kwenye BOQ jambo lililoongeza bajeti ya ujenzi na kufikia Sh bilioni 32,” alisema Killo.

Majaliwa alihoji tena; “kutoka Sh bilioni 13 hadi kufikia Sh bilioni 32, je unaona inakuja vizuri hiyo? Sh bilioni 10 hadi bilioni 13 tena, hadi Sh bilioni 32 inazungumzikaje hii na je mwenye jengo mlikubaliana naye? Awali mwenye mahitaji alisema ana Sh bilioni 10, sasa imefikaje 32 je, mlimshauri muhusika kuhusu ongezeko hili?”

Killo alipotakiwa kueleza sababu za kuongezeka gharama za ujenzi huo, alisema waligundua tofauti wakati wakiwa eneo la ujenzi kwamba kuna kazi zilitakiwa zifanyike, lakini katika mkataba hazipo na hawakuwasiliana na muhusika.

Miongoni mwa vitu vilivyosahaulika katika BOQ ya mradi huo, ni pamoja na kutokuwepo kwa ghorofa ya nne katika jengo moja wanalolijenga katika mradi huo ambalo ni la ghorofa nane, pia hapakuwa na paa la jengo la kuhifadhia vifaa mbalimbali vya NEC.

Majaliwa alisema miradi mingi inayojengwa na TBA katika maeneo mbalimbali imeshindwa kukamilika kwa wakati, hivyo amemwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama asitishe mkataba huo wa ujenzi na atafutwe mkandarasi mwingine aje amalizie.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles