25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Mkuu: Majaji marufuku kupokea amri

KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

JAJI Mkuu Profesa Ibrahim Juma amewafunda majaji mapya 12 na kuwaambia ni marufuku kupokea amri ama maelekezo ya aina yoyote ya namna ya kuendesha mashauri mahakamani au kufikia maamuzi ya kimahakama.

Profesa Juma alisema hayo Dar es Salaam jana alipofungua mafunzo ya wiki tatu ya majaji wapya yanayofanyika  Kituo cha Mafunzo Kisutu kwa wiki moja, kisha wiki mbili nyingine watamalizia mafunzo Chuo cha Mafunzo Lushoto.

“Wakati wa kazi zenu za ujaji mtakumbana na majaribu mbalimbali ya uhuru wenu, mtaweza kupambana na majaribu hayo iwapo mtabakia kwenye viapo vyenu.

“Msome kanuni zinazotoa mwongozo ambazo zinaelekeza kuwa ofisa wa mahakama Tanzania analindwa na misingi ya usawa, haki na maadili katika kazi zake.

“Kanuni ya kwanza inamtaka kila mmoja kujikinga kuingiliwa kazi, hata kutoka kwa ndugu zenu, marafiki na hata wenzenu.

“Kanuni zinaeleza kuna mazingira ambayo baadhi ya wanafamilia wanaweza kujitokeza na kutoa mwongozo wa namna ya kufanya kazi zenu, kanuni hizi zinawakumbusha msiruhusu wengine kuonyesha wako katika nafasi muhimu ya kuathiri kazi zenu,” alisema.

Alisema kanuni hizi zinazohusu uhuru wa kufanya kazi zinaenda wakati mwingine zikasababisha kujitoa kwenye shauri lililopo mbele yako ili ionekane uko huru.

“Mfano kanuni ya pili inakutaka ujiondoe kwenye shauri pale ambapo uhuru wako unaweza kuhojiwa, kuna maamuzi mbalimbali ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa, mna haki ya kupitia na kuona umuhimu wa kujitoa.

“Mfano kesi ya Mwita Chacha na wenzake iliyoamuliwa mwaka 2007 na Mahakama ya Rufani, unakumbuka jaji anaweza kujitoa pale anapoona anaweza kuegemea upande mmoja katika uamuzi wake, unapaswa kutoa sababu kwanini unajitoa.

“Ofisa wa mahakama hatakiwi kujitoa bila kutoa sababu za msingi, hii inaweza kusababisha ucheleweshaji na mzigo kwa ofisa mwingine atakyepangiwa shauri hilo.

“Utayari wa kujitoa bila sababu za kutosha ni ubakaji wa kazi za kimahakama na utachochea maombi yasiyo ya msingi kwa maofisa wa mahakama kujiondoa katika mashauri mbalimbali pale wanapoombwa na wadaawa kufanya hivyo.

“Kuna mazingira mengine majaji hutumia vibaya madaraka yao kujitoa, mfano katika kesi maarufu ya Chavda iliyoamuliwa mwaka 2016, jaji aliwasikiliza wadaiwa maombi ya kuongezewa muda, akaahirisha kutoa uamuzi kwa miezi 18, wadaiwa walipofika mbele yake alijitoa kwenye shauri hilo kwa sababu mmoja wa wadaawa alikuwa mteja wake kwenye kampuni yake ya uwakili kabla hajawa jaji,” alisema Profesa Juma.

Alisema kesi hiyo ilienda kwa marejeo Mahakama ya Rufaa, mahakama hiyo ilieleza ofisa anaweza kujitoa wakati wowote kama akibaini ana masilahi binafsi, lakini isiwe kwa sababu zisizo za msingi.

Profesa Juma alisema kuchukua muda mrefu nje ya siku 90 bila kutoa uamuzi na baadaye kugundua ana masilahi binafsi ni jambo lisilokubalika ambalo linaweza kusasababisha maamuzi ya kinidhamu kwa mujibu wa kanuni.

“Majaji wapaswa mara moja mnapopangiwa mashauri kuyasoma kwa makini ili kugundua kama kuna masilahi yoyote binafsi, sababu zingine binafsi zisiingilie jukumu lako la kudumisha uhuru, imani yako katika dini na mazoea yasiruhusiwe kuingizwa kwenye mwenendo wa mashauri na baadaye kwenye uamuzi ambao mtaufanya kama majaji.

“Mnapaswa kujifunza mara moja mazingira yanayowazunguka na namna ya kukabiliana na mashinikizo kutoka kwa majaji wengine au majaji waliopo juu yenu au wasaidizi wa kisheria.

“Kama majaji wapya mmetokea katika mazingira tofauti, mazingira hayo yanawaleta kwa pamoja, miunganiko yenu ya zamani isiwe mianya ya kuwaingilia kwenye uhuru,” alisema Profesa Juma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles