MWIMBAJI wa muziki wa injili, Rebecca Malope ambaye ni raia wa Afrika Kusini, anatarajia kuongeza nguvu katika Tamasha la Krismasi linalotarajia kufanyika Desemba 25 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama, alisema mwimbaji huyo atakuwa jukwaa moja na wenzake, Sarah K wa Kenya na Ephraim Sekeleti wa Zambia.
Msama alisema kamati yake inaendelea na mchakato wa kufanikisha tamasha hilo ambalo ni mwendelezo wa Tamasha la Amani lililofanyika Oktoba 4 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Aidha, Msama alisema Watanzania walichukilie tamasha hilo kama sehemu ya kurudisha shukrani kwa Mungu baada ya kutupitisha katika kipindi kigumu cha uchaguzi mkuu ambao ulifanyika kwa amani na utulivu ingawa kulikuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani.
Msama alisema waimbaji wa Tanzania watakaosindikiza tamasha hilo ni pamoja na Rose Muhando, Upendo Nkone, Joshua Mlelwa, Kwaya ya Wakorintho wapili huku kamati ikiendelea na mchakato wa kufanikisha tamasha hilo.