Kulwa Mzee, Dar es salaam
JAJI Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma amesema sheria inayoruhusu mshtakiwa kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) (plea bargaining), inapaswa kutumika kwa makosa mengi zaidi kwani anaamini itasaidia kupunguza msongamano magerezani.
Jaji Mkuu, Profesa Juma alisema hayo jana katika hafla ya kuwaapisha Manaibu Wasajili wa mahakama na kuwakabidhi vitendea kazi Mahakimu Wafawidhi.
Akizungumzia sheria ya makubaliano, Jaji Mkuu alisema sheria hiyo imekataza makosa machache kama mauaji, ubakaji na kwamba haitumiki kwa mashitaka ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi pekee.
“Sheria hii ilitumika Marekani na imewapa faida kubwa kwa kupunguza kesi nyingi hivyo tusilalamike sheria mbaya lakini zinarahisisha utoaji haki,” aliongeza.
Kauli hiyo ya Jaji Mkuu imekuja katika wakati ambao watuhumiwa 700 wakiwa wameandika barua kwa DPP kukiri makosa ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha, na baadhi yao wakiwa tayari wameachiwa huru kwa masharti.
Jaji Profesa Juma pia aliwataka mahakimu wasiwe wagumu kutoa dhamana kwa watanzania kwa sababu ni haki yao na wasizuie kwa matakwa yao binafsi.
Alieleza kuwa mshtakiwa akiwa kitambulisho cha Taifa apewe dhamana na endapo atakimbia maana yake atajihukumu kwa kukimbia uraia wake.
Pamoja na hayo Jaji Mkuu amewataka mahakimu kutokubali kuahirisha mashauri kwa hoja nyepesi zinazotolewa na waendesha mashtaka kwamba; ‘upelelezi wa kesi unaendelea’.
“Lazima mahakimu watumie nafasi yao kuwabana waendesha mashtaka ili waseme ni upelelezi gani unaofanywa, haukamiliki kwani ndio chanzo cha kutomaliza mashauri kwa wakati.
“Msikubali waendesha mashtaka wawatishe kwa lolote akifanya hivyo mpeleke kwa mtendaji kwa sababu kitendo hicho ni kukiuka maadili.
“Pitieni mabadiliko mbalimbali ya sheria ambayo yatatusaidia kumaliza kesi kwa wakati,” alisema.
Jaji Mkuu pia aliwataka majaji na mahakimu kujiepusha na ndugu na marafiki zao wanaotumia nafasi zao kuvunja sheria na kujinufaisha.
“Wapo baadhi ya ndugu wa majaji au mahakimu ambao wanavunja sheria kwa kuchukua mali za watu wengine kwa kutumia vyeo vya ndugu zao.
“Unakuta mke wa Jaji au hakimu anatumia nafasi ya mume wake kuliko hakimu au jaji mwenyewe hadi anaogopeka katika jamii, wengine wanachukua mali za wengine na kuvunja sheria hii si sawa kabisa,” alisema Jaji Profesa Juma.
Aidha amewataka wasitumie nafasi walizonazo kuongea na wakuu wa vituo vya polisi kwa ajili ya kuondoa mashtaka kwa ndugu zao badala yake wahakikishe wanafuata sheria kwani hakuna mtu aliye juu ya sheria.
Manaibu Wasajili walioapishwa ni Happiness Ndesamburo, Warsha Ng’humbu, Elizabeth Nyembele, Niku Mwakatobe, Arnold Kirekiano, David Ngunyale, Flora Mtarania, James Kareyamaha, Magdalena Ntandu, Chiganga Tengwa na Godfrey Isaya.
Mahakimu Wafawidhi waliokabidhiwa vitendea kazi ni Hassan Makube, Gadieli Mariki, Ebiseeza Kalegeya, Maira Kasonde, Martha Mahumbuga, Elimo Massawe, Silvia Lushashi, Monica Ndyekobora, Gabriel Ngaeje na Venance Mlingi.