27.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

Ada ya visa juu mara sita zaidi wanaokwenda kuhiji Makka

RIYADH, SAUDI ARABIA

SAUDI Arabia imeongeza ada ya visa mara sita zaidi, uamuzi ambao unatajwa kuwagharimu waumini wa madhehebu ya Kiislamu hasa wale wanaokwenda kuhiji kwa mara nyingine ambao watachajiwa zaidi.

Taarifa zinaeleza kuwa visa kwa ajili ya mtu mmoja kuingia nchini humo hivi sasa itagharimu dola za Marekani 533 ambazo ni sawa na shilingi za  Tanzania 1,226,150.64, kutoka dola 93 sawa na shilingi 213,962.03,  ya kuingia mara nyingi.

Aidha visa ya miezi sita itagharimu dola 800 takribani shilingi za Tanzania 1,840,356.64 huku ile ya mwaka mmoja itakuwa dola 1,333 ambazo ni sawa na shilingi za Tanzania 3,066,494.25.

Taarifa mbalimbali zilizoripotiwa kwenye vyombo vya habari katika nchi mbalimbali,  zimeeleza kuwa  nchi  zenye waislamu wengi zimekasirishwa na uamuzi huo.

Aidha ongezeko hilo la ada ya visa itawagusa pia watalii wote, watu wa kidini na wafanyabiashara wa kigeni.

Kwa mujibu wa ripoti ya Quartz Africa, ongezeko hilo la ada halitawagusa wale wanaosafiri kwa mara ya kwanza kutekeleza ibada ya Hija ya kila mwaka au Hija ndogo, isiyo ya lazima inayojulikana kama Umrah.

Hija inajumuisha gharama kubwa kwa wageni, hasa kwa usafirishaji na makazi.

Taarifa zinaeleza kuwa mpango huo, ambao ulitokana na mapendekezo kutoka kwa Mawaziri wa Fedha na Uchumi wa Saudia,  ulianza kutekelezwa Oktoba 2 mwaka huu  sanjari na mwanzo wa mwaka mpya wa Kiislamu.

Imeelezwa kuwa mabadiliko hayo ya ada ni sehemu ya kampeni pana ya kupunguza utegemezi wa ufalme  kwenye mafuta na kuongeza mapato katika maeneo mengine, pamoja na ada ya uhamiaji

Saudia Arabia, ambayo ndio mzalishaji mkubwa wa mafuta duniani, imeathiriwa sana na kuanguka kwa bei ya mafuta.

Septemba mwaka huu, kwa mara ya kwanza Serikali ya Saudia ilitangaza kwamba itapunguza mshahara na posho za watumishi wa umma.

Uamuzi huo ulikuja baada ya  vita vya muda mrefu huko Yemen ambavyo Saudi Arabia imehusika.

Taarifa za vyombo vya habari zinaeleza kuwa hatua ya kuongeza ada inaweza kuwa muhimu sana kwa ufalme, ikizingatiwa kwamba mamilioni ya Waislamu hufanya Hija kwenda Makka na Madina kila mwaka.

Mawakala wa usafirishaji nchini Morocco wamekubalina kususia safari za kwenda Makka hadi hapo ada hizo mpya zitakapoondolewa, ripoti  zinasema na kuongeza Uturuki, Misri, na Nigeria wote wameelezea kupinga kwao mpango huo mpya.

Waislamu nchini Afrika Kusini wameanza mchakato wa kupinga ada hizo mpya ambazo wameziita kuwa ‘si za kibinadamu’na wameitaka Serikali ya Saudia ama kuiondoa au kupunguza kiwango hicho kipya.

Yusuf Abramjee ambaye ni Katibu Mkuu wa Baraza la Wanatheolojia wa Kiislamu nchini Afrika Kusini alisema kwamba jamii inaelewa kuwa “hali ya uchumi wa dunia ni moja ya sababu” zilizoishinikiza Serikali ya Saudia ichukue hatua hizo.

” Lakini, huwezi kupata faida kutokana na Hija. Siyo sawa. Dini yetu inakataza hilo,”  hadi sasa mawasiliano na Serikali ya Saudia yalikuwa hayajafikiwa kwani simu zote za kutoa ufafanuzi zilikuwa hazijibiwi,” alikaririwa  Abramjee  akisema.

Idadi ya watu ambao huenda hija inatambuliwa na Serikali ya Saudia,  lakini imekuwa ikipungua kwa miaka michache iliyopita kutokana na sababu mbalimbali ikiwapo mipango ya upanuzi inayofanywa katika maeneo ya kuhiji, au magonjwa kama MERS, maambukizi kwa njia ya hewa au Ebola.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles