32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

CUF yataka ruhusa mikutano ya hadhara

TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimeiomba Serikali kutoa tamko la kuruhusu mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa ili waweze kuhamasisha wananchi kujiandikisha kupiga kura Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Juzi Waziri wa Nchi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, aliongeza siku tatu za kujiandikisha katika orodha ya wapigakura katika uchaguzi huo kutokana na kuwapo idadi ndogo ya wananchi waliojiandikisha.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Jaffar Mneke, alisema ni muhimu kwa Serikali kutoa tamko hilo mapema ili waandishi wasibaki vituoni bila ya kuwapo watu wa kujiandikisha.

“Serikali ikibidi itoe tamko hilo leo (jana) kuwa vyama vya siasa viko huru kisheria kufanya mikutano ya hadhara kuhamasisha kujiandikisha na kuzungumzia masuala yanayohusu nchi yao kama katiba ya nchi inavyotaka,” alisema Mneke.

Aliongeza kuwa wanaiomba Serikali iwaondoe hofu wananchi, kwamba imedhamiria kweli kuona uchaguzi unafanyika na itasimamia kwa uhuru na haki.

“Serikali iahidi kujidhibiti isiharibu mchakato wa demokrasia na kuwadhibiti watumishi wake wasijaribu kuchezea uchaguzi huu,” alisema Mneke.

Aliiomba Tamisemi izuie vitendo vya waandishi kuhama vituoni na kwenda kuandikisha majumbani kama ilivyoripotiwa katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Tanga na Dodoma.

Mneke alisema wameamua kutoa tamko hilo baada ya kufanya utafiti kwa mikoa nane na kubaini kuwapo kwa sababu mbalimbali za baadhi ya watu kutokujiandikisha.

Alisema sababu mojawapo ni kuwa wananchi hawajahamasishwa vya kutosha kama ilivyofanyika huko nyuma mwaka 2004, 2009 na 2014.

Mneke alisema wananchi walikuwa wakisukumwa na mikutano ya hadhara na harakati za kisiasa zilizofanywa na vyama vya siasa na asasi za kiraia waliokuwa wamebeba ujumbe wa kuwaeleza umuhimu wa kujiandikisha.

“Kwa sasa CCM pekee ndio kinafanya mikutano ya hadhara na harakati za kisiasa bila kubughudhiwa, hii ni miongoni mwa sababu ya wengi kushindwa kujitokeza,” alisema Mneke.

Alisema hamahama ya viongozi wakiwamo wabunge na madiwani imewafanya wananchi waamini kuwa hakuna demokrasia nchini na kujiandikisha ni kupoteza muda.

Aliongeza kuwa wakati kanuni za uchaguzi namba 371, 371, 373 na 374 zinaagiza uandikishaji unafanyika katika vituo vilivyo katika maeneo ya umma, alidai kuna baadhi ya wasimamizi wa vituo hivyo walifunga vituo na kupita majumbani na kuandikisha kwa ubaguzi.

Akizungumzia kumbukizi ya miaka 20 ya Mwalimu Julius Nyerere, Mneke alisema nchi inapokumbuka na kuenzi mazuri aliyoyafanya, ikubaliane na mawazo yake ya kuruhusu ustawi wa vyama vingi nchini.

Mneke alisema ni vyema Serikali kumuenzi Nyerere kwa kumuunga mkono katika kuruhusu uhuru wa vyama vya siasa.

Alisema chama hicho kitaendelea kuyaenzi mazuri yote aliyoyatenda Mwalimu Nyerere, hasa katika ustawi wa demokrasia na vyama vingi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles