23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 22, 2023

Contact us: [email protected]

Ukikutwa na maji ya ‘kandoro’ jela, faini inakuhusu

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

BARAZA la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limewatahadharisha na kuwaonya wauzaji rejareja wa maji na bidhaa nyingine wanaotumia mifuko laini ya plastiki, kwamba wanavunja sheria kwani mifuko hiyo pia imepigwa marufuku.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka, alisema mifuko hiyo japo imepigwa marufuku, kasi ya kuitumia inaongezeka sana na wachuuzi wanaitumia  kuuza maji na kufungia bidhaa nyingine ndogo ndogo.

Alisema maji yanayouzwa pia usalama wake kwa matumizi ya binadamu haujathibitishwa rasmi na chombo chochote.

Katika Jiji la Dar es Salaam, mifuko hiyo laini inatumika kuchuuza rejareja maji yanayoitwa ‘kandoro’ na bidhaa nyingine kama vile karanga, bisi na kadhalika.

Kiongozi huyo alisema kuwa kurudi kwa maji hayo mitaani kunatishia usalama wa afya za watu na mazingira.

 “Licha ya kwamba hiyo mifuko hairuhusiwi, hatujui maji hayo yanatoka wapi. Hali hii inahatarisha afya ya mlaji.

“Kama kweli ni mjasiriamali na unataka kuzalisha na kuuza maji, basi nenda TBS na hivyo vifungashio na maji yako, wakapime waangalie maji unazalishia eneo gani. Ukifika pale watakuratibu. Kwa sasa maji hayo hayaruhusiwi kabisa,” alisema Dk. Gwamaka.

Alisema kuwa taasisi yake ina jukumu la kuunga mkono sera za Serikali kuhusu biashara, viwanda na kuboresha maisha ya wananchi na kwa hiyo inaunga mkono wajasiriamali wabunifu na wawekezaji.

“Jukumu la pili muhimu ni kuhakikisha sheria zinafuatwa ili kulinda afya ya wananchi na mazingira. Msimamo wetu juu ya mambo haya tunaueleza wazi kabisa,” alisema.

Alisema timu ya watumishi wa NEMC ipo mtaani kukagua mazingira, hivyo atakayekutwa akitumia mifuko hiyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ikiwemo kifungo au faini kutokana na vifungu vya sheria za kutunza mazingira.

“Makamu wa Rais, mama Samia Suluhu Hassan, alikwishaeleza kwamba hayo maji hayaruhusiwi. Niwaombe Watanzania kutoa ushirikiano katika kutunza mazingira yetu kwa kutoa taarifa pale ambapo kuna uvunjifu wa sheria ya mazingira. Piga simu namba 0800110116 au andika ujumbe kwenda namba 0683540344. Simu yetu haina gharama,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sheria wa NEMC, Bernard Kongoza, alisema wanafanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi kuhakikisha sheria za mazingira zinafuatwa.

Alisema mtu atakayekiuka agizo lililotolewa na NEMC atakuwa amekiuka maagizo ya Serikali, hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

“Tunashirikiana na viongozi wa polisi wa wilaya. Hivyo mtu akikutwa anatumia mifuko hiyo tutamripoti polisi na atalazimika kufuata taratibu zilizowekwa.

“Wananchi tuachane na hii mifuko kufungashia maji na vitu vingine kwa sababu inahatarisha usalama wa afya za wananchi na inahatarisha mazingira yetu,” alisema Kongoza.

MIFUKO MBADALA ISIYOKIDHI VIGEZO

Katika hatua nyingine, Dk. Gwamaka amewaonya wanaozalisha na wanaosambaza mifuko mbadala ambayo haikidhi vigezo vilivyowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwamba watachukuliwa hatua.

Alivitaja baadhi ya vigezo kwamba ni pamoja na kuwa na uzito usiopungua 70GSM, anuani ya mzalishaji au nembo ya biashara na kuthibitishwa na TBS.

Alisema si lengo la baraza hilo kukwamisha biashara, bali usalama wa binadamu na mazingira yake ni moja ya vipaumbele vyake.

“Ni muhimu kwetu kumtambua mmiliki wa mifuko hiyo ili ikitokea tatizo kwenye suala la viwango tujue muhusika ni nani.

“Hatuwezi kukiuka viwango vilivyowekwa na ndiyo maana kuna baadhi ya mifuko imezuiliwa bandarini hadi leo kwa sababu taratibu na sheria zilizowekwa hazijafuatwa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles