Brighiter Masaki – Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Erasto Sima, amewataka wananchi wa Kinondoni kujiandikisha kwenye daftari la kupiga kura mapema ili kupata viongozi walio bora.
Akizungumza na Mtanzania mapema leo, baada ya kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura, Sima anasema kuwa ukiachana na
zoezi la kujiandikisha lililoongezwa muda hadi Alhamisi wiki hii, bado Watanzania hawajawa na mwamko.
“Ni wakati wa Watanzania kujiandikisha kwenye vituo vya makazi husika ili kukamilisha haki yako ya kumchagua kiongozi unaemtaka ili unapopata na changamoto yoyote uweze kumkimbilia na kupata msaada wa haraka,” anasema Sima.
Aidha Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za mitaa wa Manispaa ya Kinondoni, Kiduma Mageni, amewataka wakazi wa manispaa hiyo kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili wachague kiongozi anayewafaa.
Akizungumza na Mtanzania wakati alipokuwa akitembelea katika vituo vya kujiandikisha, Mageni anasema kuwa mvua iliwafanya watu kujiandikisha kwa shida, lakini wakati huu zimepungua wajitokeze kwa wingi kukamilisha zoezi hilo.
“Kituo cha Mpakani A pamoja na vingine wanaendelea kujitokeza na tunaendelea kuwahamasisha watu wajiandikishe kwa kutumia gari za matangazo. Ni haki ya kila mwananchi kujiandikisha na kumchagua kiongozi aliye bora,” anasema Mageni.