WASHINGTON, MAREKANI
RAIS Donald Trump amesema ” hakuna kama yeye” kwa kuviondoa vikosi vya Marekani katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Syria.
Lakini ametetea kikamilifu hatua ambayo imekosolewa na wengi wanaohoji kwamba inahatarisha utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati na kuhatarisha maisha ya washirika wa kikurdi nchini Syria walioisaidia Marekani kukabiliana na kundi linalojiita dola la kiislamu, IS nchini Syria.
Hata hivyo Uturuki inawataja wapiganaji hao wa Kikurdi kuwa ni magaidi na kuanzisha opareshini ya kijeshi dhidi yao.
Trump alisema kuwa Marekani haiwezi kupigana ”vita visivyokuwa na mwisho”. Trump alilitaja eneo hilo la Mashariki ya Kati kuwa eneo lisilokuwa na matumaini licha ya kuhusika kwa jeshi la Marekani kwa miaka mingi pamoja na uwekezaji wa kifedha.
Trump alisema anapeleka dola milioni 50 za msaada wa dharura kuwasaidia wakristo na watu wa madehebu mengine ya kidini yalio na jamii za wachache nchini Syria.