RAMADHAN HASSAN-DODOMA
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amesema kuna haja ya wataalamu kujifunza kwa vitendo zaidi kuliko kukaa darasani.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini hapa wakati akizindua mradi wa kuboresha mafunzo na kuwajengea uwezo wakulima wa mbogamboga na matunda.
Mradi huo unatekelezwa na Ubalozi wa Uholanzi nchini kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), na unatekelezwa katika vyuo vitatu vya ufundi ambavyo ni Uyole, Tengeru na Mahinya.
Profesa Ndalichako alisema wataalamu wengi wanatakiwa kujifunza kwa vitendo jinsi ambavyo mmea unatakiwa kuhudumiwa tangu unapopandwa hadi upovunwa, ili iwe rahisi kutoa maelekezo kwa wakulima.
“Unakuta mtu anasomea kilimo ametoka Kagera, anasoma mpaka anamaliza haijui hata korosho, lakini akimaliza anasema yeye ndio mtaalamu wa kushughulikia korosho wakati hajawahi kuuona hata mti unafananaje.
“Hivyo wataalamu wengi wawe wanajifunza kwa vitendo, mtu anapobobea aweze kushiriki katika mafunzo yake kuona hilo zao tangu linapandwa hadi kufikia hatua ya mavuno, aweze kuona hatua zote zinazotakiwa kuhudumia mmea.
“Kwa sababu huduma za mmea zinategemea pia katika ngazi ya upandaji, ni suala ambalo tunapaswa kufanya kwa vitendo,” alisema Profesa Ndalichako.
Alisema Tanzania haiwezi kujenga uchumi wa viwanda bila kuwa na kilimo cha kisasa, hivyo aliwataka wakulima nchini kulima kwa tija.
“Kinachohitajika ni tija zaidi kuliko nguvu, tunataka watu watumie maarifa kuliko nguvu, mradi huu wa kuimarisha mafunzo katika sekta ya kilimo utakuwa na faida kubwa kwetu,” alisema Profesa Ndalichako.
Awali, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), Dk. Adolf Rutayunga, alisema kwa kuzingatia umuhimu wa masomo ya ufundi, wamekuwa wakifanya juhudi kuendeleza elimu ya ufundi nchini.
Alisema tangu Nacte ianzishwe hadi sasa, imeishasajili vyuo 530 na kati ya hivyo 217 ni vya Serikali na 313 vya binafsi.
“Na hivi vimegawanyika kutokana na maeneo mbalimbali ya mafunzo kitaaluma. Kwa mfano vyuo vya biashara, elimu na mipango vipo 134 na vyuo vya Serikali 57 na binafsi vipo 67,” alisema Dk. Rutayunga.
Alisema kwa upande wa afya na sayansi shirikishi, vyuo vilivyopo ni 167 ambapo vya Serikali ni 38 na binafsi 109.
“Kwa vyuo vya sayansi na teknolojia shirikishi, hapa kuna vyuo 87 ambapo 57 ni vya Serikali na 29 ni binafsi, uwekezaji hapa ni mdogo kutokana na mahitaji ya miundombinu na vifaa,” alisema Dk. Rutayunga.
Alisema vyuo vya mafunzo ya ualimu nchini vipo 142 ambapo vya Serikali ni 44 na binafsi 68.
“Kwa ujumla kuanzia mwaka 2015 hadi 2018 vyuo vyote hivyo vinatoa jumla ya wahitimu ngazi ya stastahada 278,644. Ukiangalia hivyo vyuo tangu wakati huo si namba kubwa, kuna haja ya kuvipanua,” alisema.