25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Trump azidi kukaliwa kooni

New York, marekani

RAIS Donald Trump amewashambulia wabunge wa Chama cha Democratic, akiwatuhumu kuchochea uchunguzi dhidi yake baada ya kutoa hati ya kumtaka wakili wake binafsi kutoa nyaraka za mawasiliano na Ukraine.


Wakati Trump akimshambulia vikali Mbunge wa Chama cha Democratic, Adam Schiff na kusema anatakiwa kukamatwa kwa uhaini, Australlia imethibitisha kwamba rais huyo hivi karibuni alimwomba Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Scott Marrison na viongozi wa mataifa mengine, kumsaidia Mwanasheria Mkuu wa Marekani, William Barr kupata taarifa zitakazomsaidia kuufanya uchunguzi wa mshauri maalumu, Robert Muller kutiliwa shaka.


Muller aliongoza uchunguzi wa uingiliaji wa Urusi katika Uchaguzi Mkuu wa Marekani wa mwaka 2016.
Trump pia hakuacha kuwashambulia watoboa siri ambao madai yao yalihusu mawasiliano yake ya simu na Rais wa Ukraine, Volodymir Zelensky mwezi Julai, ambayo sasa yamesababisha kuanzishwa kwa uchunguzi wa Bunge linalodhibitiwa na Democratic wa kumshtaki.


Mwanasheria wake binafsi, Rudy Giuliani, anatajwa kuwa sehemu muhimu ya juhudi za kuiomba Ukraine kufanya uchunguzi dhidi ya familia ya mpinzani mkuu wa Trump uchaguzi ujao, Joe Biden, ambayo haijatuhumiwa kwa kufanya kosa lolote lile.


Juzi alipofanyiwa mahojiano na kituo cha utangazaji cha Fox, kuhusu hati hiyo ya Bunge, Giuliani alisema anatafakari hatua atakazozichukua.
“Ninapima njia mbadala. Nitakusanya ushahidi wangu wote pamoja na mawasiliano ya ujumbe. Sijui, ikiwa wataniruhusu nitumie kanda za video na mawasiliano niliyorekodi.


“Nilikusanya ushahidi huu wote kabla ya uchunguzi wa Muller kumalizika, kwa hivyo ilikuwa wazi kuwa jukumu langu kama wakili wa Rais, mkutano wa mwisho ambao Waukraine waliuitisha, nililifanya wakati uchunguzi ulipomalizika,” alisema.


Schiff ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kijasusi, na wenyeviti wa kamati nyingine mbili zinazoongozwa na Democratic, wametoa hati hiyo kwa Giuliani na kumpa hadi Oktoba 15 kuwa amewasilisha nyaraka hizo.


Huko Australia, Msemaji wa Serikali amethibitisha alipozungumza na kituo cha utangazaji cha ABC kwamba Trump aliwasiliana na Waziri Mkuu, Marrison, kuomba kumsaidia Mwanasheria Mkuu, Barr kupata taarifa zinazohusiana na uchunguzi wa Muller.


Kulingana na Gazeti la New York Times, lililowanukuu maofisa wawili wa Marekani ambao hawakutambulishwa, nakala ya maandishi ya mawasiliano hayo ilitolewa tu kwa kundi dogo la wasaidizi wa Trump ambao wanataka udhibiti mkali wa mawasiliano hayo.

Australia imesema iko tayari wakati wote kusaidia juhudi za kufungua njia kwenye uchunguzi wa masuala kadhaa na waziri mkuu huyo pia alikubali kufanya hivyo.


Uchunguzi mpya wa maoni uliochapishwa jana umeonyesha Wamarekani wamegawika juu ya ama kuunga mkono mashtaka dhidi ya Trump au kujiweka pembeni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles