Vigogo NSSF kizimbani kwa utakatishaji bil. 2/-

0
507

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

KAIMU Mkurugenzi wa Fedha wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Jamila Vulu na vigogo wenzake nane wa Kitengo cha Fedha, wamepandishwa kizimbani kwa uhujumu uchumi, ikiwemo kughushi, wizi na kutakatisha zaidi ya Sh bilioni 2.

Washtakiwa hao walifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon.

Wankyo aliwataja washtakiwa kuwa ni Mwandishi wa Hundi, Abdul Njozi, Meneja Uhakiki, Amir Kapera, Mhasibu, James Oigo, Mhasibu Mkuu, Hellen Peter na Mhasibu Mwandamizi anayeshughulikia matumizi, Ivonne Kimaro.

Wengine ni Mhasibu Restiana Lukwaro, Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Jamila Vulu, Kaimu Meneja Rasilimali Watu, Tikyeba Alphonce na Mhasibu Dominic Mbwete.

Wankyo alidai katika shtaka la kwanza washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Julai mosi mwaka 2016 na Septemba 4 mwaka 2017 walikula njama ya kutenda makosa ya kughushi na kutakatisha.

Shtaka la pili, washtakiwa Njozi na Akiri wanadaiwa katika kipindi hicho, wakiwa watumishi wa umma, kwenye ofisi za Makao Makuu ya NSSF, walighushi hundi 47 za Benki ya CRDB kwa akaunti namba 01j1028249500 yenye jina la NSSF zenye thamani ya Sh 2,130,211,437.35.

Katika shtaka la tatu, washtakiwa wote wanadaiwa katika kipindi hicho, wakiwa Makao Makuu ya Shirika waliiba fedha hizo.

Washtakiwa hao pia wanashtakiwa kwa kosa la kusababisha hasara ya Sh 2,130,211,437.35 kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao wakiwa watumishi wa umma.

Shtaka la mwisho kwa washtakiwa wote, wanadaiwa kutakatisha kiasi hicho cha fedha huku wakijua fedha hizo zimetokana na mazalia ya fedha za kughushi.

Hakimu Mhina aliwafahamisha washtakiwa kwamba hawatakiwi kujibu lolote sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo wala kutoa dhamana kwa washtakiwa.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Oktoba 15 kwa kutajwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here