OSCAR ASSENGA, TANGA
Wizara ya Nishati imesisitiza kwamba mradi wa bomba la mafuta kutoka hoima nchini Uganda hadi Tanzania eneo la Chongoleani mkoani Tanga bado upo na unaendelea kutekelezwa baada ya tofauti ya Uganda na wawekezaji.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mratibu wa Mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Wizara ya Nishati, Salum Mnuna wakati wa kikao cha kutoa mrejesho kwa watendaji wa mkoa, wilaya na serikali za vijiji kuhusu mradi huo.
Amesema kuwa tofauti ya Uganda na wawekezaji ilitokea katika manunuzi ya hisa za moja ya waombaji wa kampuni ya dalo kukamilishwa huku akieleza kwamba kuna kazi zimesimama lakini kazi za msingi zimekamilishwa ikiwemo usanifu wa mradi, utambuzi wa njia.
Awali akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella alisema kwamba mradi unaelekea kwenye hatua ya kutwaliwa ardhi pamoja na hatua hiyo kufikiwa lakini kumekuwa na changamoto kwa wenzao wa Uganda.
Alisema changamoto hizo ni za kawaida kwenye miradi mikubwa hivyo serikali imewahakikishia zitashughulikiwa ikiwezekana mwakani shughuli zote za msingi ziwe zimekamilika na ujenzi uanze.
“Ndugu zangu washiriki kwenye mkutano huu tuende kuwafikishia ujumbe huu wananchi ambao mradi utapita waendelee kuwa na subira mradi unakuja wajiande kunufaika na fursa za bomba”.
“Lakini nisisitize kwamba fursa za ajira na nyengine bado hazijaanza rasmi kwa sababu utekelezaji wake upo hatua ya mwanzo, pasipatikane watu ambao wanatangaza fursa za ajiraza bomba la mafuta,” amesema Shigella.