TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM
CHAMA Cha ACT Wazalendo, kimeanza harakati za ndani kumuandaa Mshauri Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad kuwa mgombea urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Wakati ACT ikieleza hayo CCM kimesema kuwa suala la utabiri kwa Maalim Seif, haukuanza leo kwani ulianza tangu wakati wa Rais wa Pili wa Zanzibar, Abood Jumbe Maalim lakini katu chama hicho tawala hawashituki nao.
Akizungumza katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama hicho, Naibu Kiongozi wa ACT Wazalendo, Juma Haji Duni alisema Maalim Seif ameanza siasa 1992 akiwa kijana lakini mpaka sasa ana uwezo wa kugombea urais.
“Tulianza siasa tukiwa vijana mpaka tunazeeka lakini Maalimu Seif bado handsome ana uwezo mkubwa wa kugombea tena na tukashinda,” alisema Duni.
Pamoja na hilo alisema kuwa inatia moyo kwani wameamua kufanya kazi kwa ajili ya wananchi na si kwa ajili ya masilahi binafsi na wako pamoja kuhakikisha Watanzania wanapata haki na demokrasia nchini.
Naye Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe alisema wanashukuru wajumbe wa halmashauri kuu kwani kwa sasa chama hicho kimepata uwakilishi mzuri wa pande zote mbili Muungano na kimekuwa kuliko vyama vyote nchini.
“Nataka kuwatumia salamu CCM Zanzibar kuwa ACT ndiyo chama kitakachochukua urais 2020,” alisema Zitto.
Alisema wanajua bado wanavutana kutafuta mtu wa kugombea nafasi hiyo wao tayari wamejiimarisha kuchukua nafasi hiyo.
“Wakusanyane wote wawe kumi wanaotaka kugombea sisi tutawapiga tu,” alisema Zitto
Kiongozi huyo wa ACT aliwapa wajumbe hao salamu kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ambaye kwa sasa yupo nchini Ubelgiji kwa matibabu na kusema kuwa wako pamoja naye katika kuwatumikia wananchi.
Aliwataka wajumbe hao kujipanga katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji kwa kuhakikisha kila eneo linakuwa na wagombea wa nafasi za uenyekiti na ujumbe.
“Msiogope kwa kuwa hakuna wakati mzuri wa kupata ushindi kama tunakokwenda, wakati wao wanakuja na picha za miradi mikubwa ya ndege, madaraja, ninyi nendeni na shida za wananchi kama vile njaa, elimu, ukosefu wa ajira kwa vijana,” alisema Zitto.
Aliwataka waepuke kujiingiza katika migogoro ya ndani ya chama na nje ya vyama hasa kwa wenzao wa upinzani kwa kuwa ni njia inayotumiwa na wapinzani wao kujiimarisha.
“Leo tunafurahia kupata wanachama wengi kutoka chama kingine lakini si afya kwa vyama vyetu, hivyo lazima tuwe na udhibiti wa kuhakikisha hatuingiliwi nao,” alisema Zitto.
KAULI YA CCM
Akizungumza na MTANZANIA, Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao, alisema suala la kumtabiria Maalim Seif kuwa Rais wa Zanzibar halikuwa anza leo kwani lilianza tangu utawala wa Rais wa Pili Abood Jumbe Maalim.
Alisema pamoja na hali hiyo bado ACT wanatakiwa kutafuta utabiri mwingine dhidi ya Maalim Seif lakini si urais kwani kwa sasa Zanzibar Rais ni Dk. Ali Mohamed Shein
“Kwa sasa Zanzibar Rais ni Dk. Shein na CCM haina mgombea kwani huwezi kuwa na mgombea hali ya kuwa Rais yupo. Na itakapofika mwaka 2020 nasi tutatangaza utaratibu wetu ndani ya chama ambapo tutapata mgombea ambaye atakuwa mzuri na kwenda kwa wananchi na ninaimani tutashinda.
“Utabiri dhidi ya huyo mtu (Maalim Seif) haukuanza leo wala jana, ila pamoja na yote bado wanaendelea na sasa imefika tena wabadili watabiri ila CCM iko imara wakati wote na hatuna shaka.
“Mara zote alizogombea nafikiri majibu ya utabiri wao majibu waliyapata na wataendelea kuyapata kwa sababu wananchi wanajua,” alisema Nao